TAARIFA YA MKUTANO WA 8 WA BUNGE (UNGE LA BAJETI)



1.0       UTANGULIZI:
 Mkutano wa Nane wa Bunge unatarajiwa kuanza tarehe 12 Juni, 2012 na kumaliza shughuli zake tarehe 22 Agosti, 2012. Mkutano huu utakuwa na shughuli mbalimbali kama vile Kiapo cha Utii kwa Waheshimiwa Wabunge wateule, kujadili Makadirio ya matumizi na mapato ya serikali kwa mwaka wa fedha 2012/2013, Maswali kwa Waziri Mkuu na Maswali ya kawaida pamoja na chaguzi mbalimbali ili kujaza nafasi zilizoachwa wazi baada ya uteuzi wa Mheshimiwa Rais kwa baadhi ya wabunge kuingia katika Baraza la Mawaziri.

2.0         MUDA WA MKUTANO WA NANE WA BUNGE:
Kanuni ya 97(1) ya Kanuni za Bunge Toleo la Mwaka 2007, imeweka kiwango cha juu cha siku zitakazotumika kwa ajili ya mjadala wa Hotuba ya Bajeti ya Serikali kuwa ni siku tano. Pia, Kanuni ya 99(1) imeweka kiwango cha siku zisizozidi hamsini kwa ajili ya Bunge kujadili utekelezaji wa Wizara zote za Serikali.
Hivyo basi katika Mkutano huu wa Nane jumla ya siku nne (4) zimetengwa kwa ajili ya kujadili na kupitisha Bajeti ya Serikali, na jumla siku aronbaini (40) zimetengwa kwa ajili ya kujadili utekelezaji wa Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara nyingine zote.

3.0    SHUGHULI ZA SERIKALI:
Kwa mujibu wa Kanuni 17 (1) (d) ya Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la 2007, Shughuli ambazo zitatekelezwa katika Mkutano huu utakaokuwa wa siku 49 za kazi ni kama ifuatavyo:

3.1.      KIAPO CHA UTII:
Kwa mujibu wa Kanuni ya 24 ya Kanuni za Bunge, Toleo la 2007 na kufuatia uteuzi uliofanywa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mujibu wa masharti ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 66 (1) (e) kutakuwa na kiapo cha Utii kwa Wabunge wateule wafuatao:-
1.    Mhe. James Francis Mbatia;
2.    Mhe. Janet Zebedayo Mbene;
3.    Mhe. Prof. Sospeter Mwijarubi Muhongo; na
4.    Mhe. Saada Mkuya Salum.

3.2       Miswada ya Sheria:
Miswada ya Sheria itakayosomwa kwa Mara ya Kwanza na hatua zake zote: [Chini ya Kanuni ya 83 ya Kanuni za Bunge] ni kama ifuatavyo:
·         Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2012 (The Finance Bill, 2012).
·         Muswada Sheria ya Kuidhinisha Matumizi ya Serikali wa Mwaka 2012 (The Appropriation Bill, 2012).

3.3       Kujadili Bajeti:
Majadiliano ya Bajeti ya Serikali yanaongozwa na Kanuni zilizopo katika Sehemu ya Tisa ya Kanuni za Bunge inayohusu Utaratibu wa Kutunga Sheria kuhusu mambo ya Fedha. Kanuni ya 96(2) inaelekeza kuwa Hotuba ya Bajeti lazima iwasilishwe Bungeni na Waziri wa Fedha kabla ya tarehe 20 mwezi Juni kwa kila Mwaka.

Kutokana na kanuni hiyo, Bajeti  ya  Serikali  itasomwa  siku  ya  alhamisi  tarehe  14 Juni 2012 ambapo Nchi zote za Afrika Mashariki zitasoma Bajeti zao kama ambavyo walisha kubaliana.

Katika siku hiyo baada ya kipindi cha Maswali, Waziri anayehusika na Mipango atawasilisha na kusoma hotuba yake ya Hali ya Uchumi wa nchi na jioni kuanzia saa 10.00 Waziri wa Fedha atasoma Hotuba ya Bajeti ya Serikali.

Kutokana na Utamaduni wetu baada ya kusoma Bajeti hiyo Bunge litaahirishwa kwa siku moja kwa lengo la kuwapatia Wabunge nafasi ya kusoma na kutafakari Hotuba ya Hali ya Uchumi na Hotuba ya Bajeti ya Serikali na kujiandaa kwa majadiliano yatakayoanza tarehe 18 Juni, 2012 hadi tarehe 21 Juni, 2012.

Kwa Mujibu wa Kanuni ya 98 (2) Siku ya Alhamisi tarehe 21 Juni, 2012, Bunge litapiga kura ya uamuzi wa Bajeti ya Serikali. Siku hii ni muhimu sana kwa Wabunge wote kuwa Ukumbini kwa sababu kura hupigwa kwa kuita majina.

Tarehe 22 Juni, 2012 Bunge litajadili na kupitisha Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2012 (The Finance Bill, 2012). Tarehe 25 hadi 29 Juni, 2012 kwa muda wa siku tano kutakuwa na mjadala wa Hotuba ya Waziri Mkuu juu ya utekelezaji wa Shughuli za Serikali katika Mwaka wa Fedha unaomalizika, na matarajio ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha unaofuata. Mjadala wa Hotuba za Mafungu ya Wizara nyingine utaanza tarehe 02 Julai, 2012 kwa mtiririko kama unavyoonekana kwenye ratiba hadi tarehe 20 Agosti, 2012.

4.0       SHUGHULI NYINGINE:
      4.1    MASWALI:
      (i)         Maswali ya Kawaida:
(Chini ya Kanuni ya 39(1) ya Kanuni za Bunge, Toleo la 2007):
Itakumbukwa kuwa, nyakati za vikao vya Bajeti, Maswali yanayowekwa kwenye orodha ya Shughuli za Bunge ni kumi tu kwa siku za kawaida na matano siku za Alhamisi, Hivyo, katika Mkutano huu inatarajiwa kuwa, Maswali 454 yataulizwa na kujibiwa.

(ii)        Maswali kwa Waziri Mkuu:
(Chini ya Kanuni ya 38(1) ya Kanuni za Bunge, Toleo la 2007):
Utaratibu wa kumuuliza Maswali Mheshimiwa Waziri Mkuu kila Alhamisi kama tulivyokubaliana utaendelea na inakadiriwa kuwa maswali yasiyopungua 64 yataulizwa.

4.2       UCHAGUZI WA MWENYEKITI WA BUNGE:
Kwa mujibu wa Kanuni ya 11 ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la 2007 kutakuwa na uchaguzi wa Mwenyekiti wa Bunge  ili kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Mheshimiwa George Boniface Simbachawene (Mb) aliyeteuliwa na Mheshimiwa Rais kuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Nishati na Madini.

4.3.      UCHAGUZI WA MJUMBE WA BUNGE LA AFRIKA:
Kwa mujibu wa Kanuni ya 12 ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la 2007 kutakuwa na uchaguzi wa mjumbe wa Bunge la Afrika ili kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Mheshimiwa Stephen Julius Massele (Mb) aliyeteuliwa na Mheshimiwa Rais kuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Nishati na Madini.

Imetolewa na :
Idara ya Habari, Elimu kwa Umma
na Uhusiano wa Kimataifa
Ofisi ya Bunge
DAR ES SALAAM
Tarehe 8, Juni, 2012