AFYA
ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk Steven Ulimboka imeendelea
kuimarika baada ya kupata matibabu nchini Afrika Kusini na sasa figo
zake zimeanza kufanya kazi.Dk Ulimboka alipelekwa nchini huko mwishoni
mwa wiki baada ya kushambuliwa na watu wasiojulikana kiasi cha
kusababisha figo zake kushindwa kufanya kazi.Katibu wa Chama cha
Madaktari Tanzania (MAT), Dk Rodrick Kabangila alisema Dar es Salaam
jana kwamba, hali ya Dk Ulimboka imeimarika na kuwaomba Watanzania
wamuombee apone haraka.“Taarifa tulizozipata kutoka Afrika Kusini
zinasema kwamba, hali ya Dk Ulimboka imezidi kuimarika tofauti na
alivyokwenda, figo zimeanza kufanya kazi ingawa kwa polepole na
amefanyiwa vipimo vingine,” alisema Dk Kabangila na kuongeza:
“Pia ameanza kuzungumza, anawatambua watu vizuri na zaidi amewaomba Watanzania wamuombee apone haraka.”
Awali,
chanzo kimoja cha habari kilidokeza kwamba hali ya Dk Ulimboka
imeimarika kutokana na kupatiwa huduma za matibabu kwa haraka kwa
kufanyiwa pamoja na vipimo vingine, kile cha usafishaji damu na figo
(Dalysis), mara kwa mara. Kabla ya kuondoka nchini, Dk Ulimboka
alifanyiwa usafishaji huo mara mbili.
Madaktari
walisema kuwa, kipimo hicho kililenga kupunguza kiwango cha sumu
iliyoonekana kwenye damu, ambayo haikutambulika mara moja kama
ilitengenezwa ndani ya mwili au vinginevyo kwa kuwa hakuna kipimo cha
kubaini tatizo hilo nchini.
Migomo hospitalini
Licha
ya huduma kurejea taratibu katika baadhi ya hospitali nchini, mgomo wa
madaktari bingwa umeendelea chini kwa chini.Pia jana, Serikali imewataka
madaktari wote walio katika mafunzo ya vitendo kuripoti Wizara ya Afya
na Ustawi wa Jamii, ifikapo Ijumaa.
Jana,
wizara hiyo ilitoa taarifa ikitaka madaktari wote nchini wanaofanya
mafunzo kwa vitendo (interns) ambao walipewa barua za kurudishwa
wizarani, kuripoti Dar es Salaam Julai 6, mwaka huu.
Mgomo
wa madaktari bingwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH),
umekuwa na utata baada ya kuwapo taarifa mbili zinazokinzana.
Uongozi
wa (MNH) kupitia kwa Msemaji wake, Aminiel Aliegaeshi umetoa taarifa
kwa umma kupitia vyombo vya habari jana ukisema huduma za matibabu
zinaendelea kama kawaida, lakini kwa kiwango cha kati.
“Huduma
hapa hospitalini zinaendelea kutolewa kwa kiwango cha kati, wagonjwa ni
wachache wanaokuja kutibiwa. Madaktari Bingwa wote wameingia na
kufanya kazi na Interns kumi na moja wamefanya kazi,” alisema.
Jana
waandishi wetu walishuhudia baadhi ya huduma zikiendelea kutolewa kama
kawaida katika hospitali hiyo zikiwemo x-ray katika Taasisi ya Mifupa
(Moi) na hospitali hiyo kuu.
Awali, huduma hiyo na nyingine zilisimama baada ya tukio la kutekwa na kupigwa kwa Dk Ulimboka.
Lakini,
wakati Aliegesha akitoa taarifa hiyo, madaktari bingwa wamesisitiza
kuwa wako kwenye mgomo huku msemaji wao, Dk Cathrine Mng’ong’o akitaka
waandishi wa habari kulinganisha maneno hayo ya uongozi na hali halisi
hospitalini hapo.
“Mimi
siwezi kujibu swali hilo (kama wako kwenye mgomo au wamerudi), sababu
sipo katika eneo la hospitali leo, niko nyumbani. Wewe angalia kwa
macho yako uone kisha linganisha maneno hayo na hali halisi,” alisema Dk
Mng’ong’o.Alipoulizwa kuwa kama jana alikuwa zamu alijibu kwa kifupi
kuwa madaktari bingwa hawana zamu na hufanya kazi saa 24.
Madaktari hao juzi walitangaza mgomo wakitaka Serikali kuwarudisha kazini madaktari wote waliofukuzwa.
Uongozi
wa MNH ulisema, idara ambazo madaktari walikuwapo ni ya huduma za
dharura na katika vitengo vingine ilidaiwa kuwa walifika kwa kiwango
kikubwa.
Katika
Hospitali ya Mkoa wa Arusha, Mount Meru, hali imezidi kuwa tete baada
ya wagonjwa kuhamishiwa hospitali za binafsi kutokana na kuzorota kwa
huduma.Mkazi wa Sakina aliyejitambulisha kwa jina moja la Manka, ambaye
mtoto wake alikuwa amelazwa hospitalini hapo akisubiri upasuaji alisema,
amelazimika kumhamisha mtoto wake kutokana na kukosa huduma.
Hata
hivyo, Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Eliringia Mlay alikanusha
madai ya kuwapo kwa mgomo hospitalini hapo na kusema kuwa, ulikuwapo
awali lakini kwa sasa umekwisha na madaktari wanaendelea na kazi kama
kawaida. Hospitali binafsi
Hospitali
ya TMJ imeanza kutoa huduma ya tiba kwa baadhi ya wagonjwa waliokuwa
Muhimbili baada ya kuingia mkataba na Serikali ili kutoa huduma ya
matibabu katika kipindi ambacho madaktari wa Serikali wapo katika mgomo.
Msemaji
wa Hospitali hiyo, Huzaifa Seif alisema jana kuwa wagonjwa wanaotibiwa
katika hospitali hiyo ni wale wenye kadi za Bima ya Afya na wagonjwa
walioandikiwa rufaa kutoka MNH.
Hata
hivyo, mmoja wa wagonjwa, Anaeli Mbasha alisema ingawa Serikali
imeingia mkataba na hospitali hiyo, wagonjwa wengine wenye kipato kidogo
wanashindwa kuhimili malipo.
Hospitali
ya Regency imekuwa na ongezeko la wagonjwa ikiaminika kuwa ni kutokana
na mgomo huo wa madaktari. Mmoja wa madaktari hospitalini hapo, Dk
Emmanuel Jonathan alisema wagonjwa ni wengi hasa kutoka Muhimbili.
Katika
Hospitali ya Aga Khan, baada ya wiki iliyopita kuwa na ongezeko la
wagonjwa kwa asilimia 15, idadi hiyo imepungua kati ya jana na
juzi.Mkurugenzi wa Tiba wa Aga Khan, Dk Jaffer Dharsee alisema:
“Ongezeko kubwa lilikuwa katika vipimo ambavyo vinapatikana katika
Hospitali ya Muhimbili na hapa (Aga Khan), peke yake kwa mfano MRI
(Magnetic Resonance Imaging).”
Geofrey
Nyang'oro, Victoria Mhagama, Halima Shebuge, Zakhia Abdallah, Sam Jacob
(SJMC), Pamela Chilongola na Sam Jacob, Moses Mashalla, Arusha.