AGIZO
la Rais Jakaya Kikwete kuwataka madaktari wanaoendelea na mgomo kuacha
kazi limechukua sura mpya baada ya madaktari bingwa ambao awali
hawakuhusika kabisa na mgomo huo, kutoa tamko wakimtaka kiongozi huyo wa
nchi kuwatimua wao kwanza kabla ya wale wa ngazi ya chini.
Badala yake, madaktari bingwa ambao walitangaza kujiunga na wenzao
juzi, baada ya kupigwa na kujeruhiwa vibaya kwa Dk. Steven Ulimboka,
walisema wataendelea na mgomo wao hadi hapo serikali itakapowarejesha
kazini madaktari na madaktari wanafunzi wote waliofukuzwa.
Akitoa tamko la madaktari bingwa waliokutana kwa dharura jana na
kamati ya jumuiya ya madaktari kujadili hotuba ya rais Kikwete, kiongozi
wa mabingwa hao Dk. Catherine Mng’ong’o alisema huo ni msimamo wa
madaktari wenzake, huku akitaka kufunguliwa kwa meza ya majadiliano ya
dhati yenye nia ya kumaliza mgogoro wao.
“Madaktari bingwa hatuwezi kufanya kazi bila madaktari wa chini yetu…
kama serikali imedhamiria kuwafukuza kazi hawa na interns (waliopo
kwenye mafunzo ya vitendo) ianze na sisi.
“Tuko tayari kufukuzwa iwapo madai yetu ya msingi hayatatekelezwa na
kama kuondoka waanze kutufukuza sisi kwanza,” alisema Dk. Mng’ong’o
baada ya kumalizika kwa kikao cha madaktari bingwa kilichoketi kwa zaidi
ya saa tano kwenye viunga vya hospitali hiyo.
Soma zaidi:http://freemedia.co.tz/daima/habari.php?id=37661