MESSI AUMIA MAZOEZINI.

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Argentina na klabu ya Barcelona, Lionel Messi ameshindwa kusafiri na timu hiyo kuelekea Ujerumani kwenye sherehe za miaka 125 ya klabu ya Hamburg baada ya kuumia wakati wa mazoezi. Katika taarifa iliyotolewa katika tovuti ya klabu hiyo imesema kuwa mchezaji huyo alipata mchubuko katika goti lake ambapo baada ya kufanyiwa ultrasound ilionyesha kuwa pia amepata maumivu ndani ya msuli. Messi alitarajiwa kuwa sehemu ya kivutio katika mchezo baina ya timu hizo unaotarajiwa kuchezwa baadae leo kutokana na kuendelea kukosa kwa mshambuliaji nyota wa klabu hiyo David Villa ambaye bado anapona majeraha baada ya kuvunjika mguu. Katika mchezo huo ambao unatarajiwa kuchezwa katika Uwanja wa Imtech Arena, utakuwa ni wa kwanza kwa kocha Tito Vilanova toka achukue mikoba ya kuinoa klabu hiyo kutoka kwa Pep Guardiola. Barcelona inatarajiwa kucheza michezo mitano ya kirafiki kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa Ligi Kuu nchini Hispania inayojulikana kma La Liga.