JK ashiriki katika mazishi ya kada wa CCM mzee Azzan Ally Mangushi

-Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akishiriki katika mazishi ya kada wa CCM mzee Azzan Ally Mangushi yaliyofanyika katika makaburi ya Kisutu jijini Dar es Salaam leo mchana. Mzee Mangushi aliwahi pia kuwa mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM wilaya ya Kinondoni. 
Picha na mdau Freddy Maro wa Ikulu.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete mchana wa leo, Jumanne, Julai 24, 2012, ameungana na mamia ya waombolezaji katika kumzika kada maarufu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Ndugu Azzan Ally Mangushi kwenye makaburi ya Kisutu, Dar Es Salaam.
Rais Kikwete amewasili kwenye makaburi hayo ya Kisutu, katikati ya Jiji la Dar es Salaam, kiasi cha saa saba na dakika 45 kujiunga na mamia ya waombolezaji kumzika Ndugu Mangushi ambaye alikuwa Mjumbe wa Halmashauri ya Mkoa ya Chama cha Mapinduzi.
Mbali na wananchi wa kawaida na wanachama wa CCM, mazishi hayo pia yamehudhuriwa na wanachama wa Klabu ya Soka la Simba ya Dar es Salaam ambako alikuwa mwanachama na mhamasishaji hodari.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
24 Julai, 2012