SIKU
moja baada ya Rais Jakaya Kikwete kusema daktari anayeona kuwa hawezi
kufanya kazi serikalini bila ya kulipwa mshahara wa Sh3.5 milioni aache
kazi, viongozi wa dini, wanasiasa, wabunge na wasomi wamemtaka apunguze
jazba.Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana walisema mgogoro wa
madaktari na Serikali bado unajadilika huku Mbunge wa Ubungo (Chadema),
John Mnyika akienda mbali zaidi na kusema Serikali iache kisingizio cha
Mahakama kulizuia Bunge kujadili mgogoro baina yake na madaktari, wakati
yenyewe inajadili na kutoa maelezo.
Juzi,
katika hotuba yake ya kila mwisho wa mwezi, Rais Kikwete alisema
Serikali haiwezi kuahidi kuwa inao uwezo wa kuwalipa madaktari mshahara
huo na posho zote kwani ikifanya hivyo malipo ya daktari anayeanza kazi
yatakuwa Sh7.7 milioni kwa mwezi kitu ambacho hakiwezekani.
Jana,
wakizungumza kwa nyakati tofauti, wadau hao walisema mgogoro huo kati
ya Serikali na madaktari bado unajadilika na kusisitiza kuwa hotuba ya
Rais Kikwete haijajibu madai ya madaktari.
Mhadhiri
wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Bashiru Ally alisema ingekuwa
jambo jema kama kungekuwa na uwezekano wa mazungumzo kuendelea.
Alisema kauli ya Rais ni upande wa Serikali hivyo, ingekuwa vyema kama madaktari nao wangepata nafasi ya kujieleza.
Wanasiasa
Mbunge
wa Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi), Moses Machali alimtaka Rais apunguze
hasira na kuitaka Serikali ikubali kurudi katika meza ya mazungumzo hata
kama ndiyo iliyokuwa ya kwanza kuwapeleka mahakamani madaktari
waliogoma.
Alisema
kama Serikali haiwezi kulipa kiwango cha mshahara kilichopendekezwa na
madaktari, irudi katika meza ya mazungumzo ili kutafuta suluhu ya mgomo
huo unaowaumiza zaidi wananchi.
“Warudi
kwenye meza ya majadiliano siyo kila mmoja kusema la kwake na kuacha
mgomo kuendelea huku, watu wakiteseka hospitalini bila msaada wowote,’’
alisema Machali.
Naibu
Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Julius Mtatiro alisema
Serikali haipaswi kuwafukuza madaktari kwa kuwa imetumia gharama kubwa
kuwasomesha.
“Ikiwafukuza madaktari italazimika kuwaleta walio nje ya nchi ambao ni gharama kubwa… Serikali itatue mgogoro huu,” alisema.
Mbunge
wa Ubungo (Chadema), John Mnyika alisema Serikali iache kutumia
kisingizio cha Mahakama kulizuia Bunge kujadili mgogoro wa madaktari
wakati yenyewe ikitoa ufafanuzi.
“Uamuzi
wa Serikali kutoa kauli kupitia hotuba ya Rais una mwelekeo wa kukwepa
wabunge kujadili hotuba husika ambayo awali, ilielezwa kuwa ingetolewa
na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda bungeni. Inawanyima haki wabunge
wasitimize wajibu wa kikatiba wa Ibara 63 (2) wa kuisimamia Serikali kwa
niaba ya wananchi,” alisema Mnyika.
Mnyika
alisema, kwa kuwa Bunge litajadili mapitio ya utekelezaji wa Bajeti ya
Ofisi ya Rais kwa mwaka wa fedha 2011/2012 na makadirio ya mapato na
matumizi kwa mwaka wa fedha 2012/2013 kuanzia leo, ni muhimu wabunge
wakajadili pia masuala ambayo Rais ameyaeleza kwa taifa na kutimiza
wajibu wa kikatiba.
“Hotuba
ya Rais imeendeleza kauli za upande mmoja ambazo zimekuwa zikitolewa na
Serikali kuhusu mgogoro huo bila taifa kupewa fursa ya kupata maelezo
na vielelezo vya upande wa pili, hivyo Serikali imetoa kauli yake
hadharani badala ya bungeni au mahakamani.
Viongozi wa dini
Mchungaji
wa Kanisa la Maombezi (GRC) Ubungo Kibangu, Anthony Lusekelo alisema
madaktari hao wanatakiwa kurudi kazini kwa kuwa tayari Serikali
imeshasema kuwa haina fedha za kuwalipa na kuongeza kuwa hata kama wana
madai yao, wadai wakiwa kazini.
“Asilimia
kubwa ya madaktari wamesomeshwa na Serikali… Serikali hiyohiyo
inawaeleza kuwa haina fedha za kuwalipa kama wanavyotaka, binafsi
nawaomba tu warudi kazini kwa kuwa mgomo wao unawaathiri zaidi wananchi
kuliko hata hao viongozi wa Serikali.
“Tunajua
tulikotoka ila hatujui tunakokwenda, kama ni kuboreshwa kwa sekta nzima
ya afya, Serikali imesema itatekeleza hilo, haiwezi kuyatekeleza kwa
siku moja, haya mambo yanajadilika.
Alisema
kama Serikali itakuwa na makosa yake, itayajibu mbele za Mungu...
“Madaktari watekeleze wajibu wa kazi yao kwa uwezo wa Serikali iliyopo
madarakani.”
Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Kagera, Dk Methodius Kilaini alisema kanisa hilo haliwezi kuunga mkono mgomo huo.
Alisema pamoja na kuwa madaktari wana madai yao, jukumu lao kubwa ni kufuata maadili ya kazi yao ambayo hayawaruhusu kugoma.
Katibu
Mkuu wa Makanisa ya Kipentekoste Tanzania, Askofu David Mwasota alisema
madaktari wanatakiwa kutenganisha siasa na maadili ya kazi yao.
“Hata
kama Serikali ina makosa yake lakini, wao kuendelea kugoma si jambo
zuri kwa jamii na hata mbele za Mungu, watumie njia nyingine kudai madai
yao, lakini waendelee kutoa huduma. Madaktari ni watu muhimu, kurudisha
viungo vya binadamu katika hali ya kawaida si kazi ndogo, warudi kazini
kuokoa mamia ya Watanzania maskini.”
Katibu
wa Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata), Mkoa wa Arusha
Abdulkarim Jonjo alisema ipo haja kwa Serikali kukaa meza moja na
madaktari hao.
Askofu
Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya
Mjini Kati, Thomas Laizer alisema mgogoro wa madaktari umalizwe kwa
mazungumzo.
Alisema
Serikali inapaswa kuwa wazi inapozungumza na madaktari kwa kueleza ni
mambo gani yanawezekana na kwa muda gani ili, kuondoa migogoro.
Akizungumza
juzi katika ibada maalumu katika kanisa la KKKT Kimandolu, alisema ili
kuondoa hisia kuwa Serikali inahusika na tukio la kutekwa Dk Ulimboka ni
lazima iundwe tume huru.
“Nadhani
ili kuondoa haya maneno ambayo si jambo dogo, Serikali inapaswa kuunda
tume huru kuchunguza tukio hili, kwani inawezekana waliohusika ni watu
wengine tu wenye nia mbaya na Serikali lakini ili ukweli ujulikane ni
muhimu kuwepo tume huru,” alisema Askofu Laizer.
Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhaj Mussa Salum aliwataka madaktari kutii agizo lililotolewa na Mahakama kwa kurudi kazini.
“Rais
ameshaeleza wazi kwamba Serikali haina fedha za kuwalipa kama
wanavyotaka, warudi tu kazini na kuweka masilahi ya Watanzania mbele na
kuacha kutanguliza masilahi binafsi,” alisema Sheikh Salum.
Wanaharakati
Mkurungezi
Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen
Kijo-Bisimba alisema hotuba hiyo ya Rais haina jipya zaidi ya kurudia
maelezo yake ya awali alipokutana na Wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam.
“Nilitarajia
kuwa hotuba itakuwa tofauti lakini sivyo. Amerudia maelezo yaleyale
aliyoyasema Machi 12 (mwaka huu) alipokutana na wazee katika Ukumbi wa
Diamond Jubilee,” alisema Bisimba.
Wakili
Peter Jonathan alisema kama kweli Serikali inataka kurudisha imani kwa
Watanzania kuhusu tukio la Dk Ulimboka ni lazima ijisafishe kwa kuunda
tume huru nje ya Serikali.
“Watafute
hata Jaji mstaafu, si lazima atoke Tanzania kuongoza tume huru ikibidi
tuchukue hata nje ya nchi ili wakitoa taarifa iweze kuaminiwa na jamii
na hiyo ndiyo dhana sahihi ya utawala bora,” alisema.
Mjumbe
wa Chama cha Watabibu wa Tiba Asili (ATME), Boniventure Mwalongo
ameitaka Serikali kuacha kutumia nguvu kushughulikia madai ya madaktari
badala yake ipanue wigo wa majadiliano ili kutatua tatizo hilo.
“Nimesikiliza
hotuba ya Rais lakini, haijaonyesha kama kuna jawabu la mgomo hivyo
wapanue wigo wa majadiliano ili kumaliza mgogoro huu,” alisema Mwalongo.
Habari hii imeandikwa na Fidelis Butahe,
Nora
Damian, Bakari Kiango, Freddy Azzah, Daniel Mwingira, Dar; Daniel
Mjema, Moshi; Mussa Juma, Arusha na Frederick Katulanda, Mwanza.
Chanzo: http://www.mwananchi.co.tz