MOURINHO KUMUUZA KAKA ILI AMPATE MODRIC.
KLABU ya Real Madrid ya
Hispania inajaribu kumuuza kiungo wake nyota Kaka kwenda AC Milan ya
Italia kabla ya kumalizia hatua za mwisho za kumyanyakuwa kiungo wa
Tottenham Hotspurs ya Uingereza, Luka Modric. Meneja wa Tottenham
Andre Villas-Boas amesema wiki iliyopita kuwa anataka sakata la uhamisho
wa mchezo huyo limalizike haraka ili aweze kuendelea na mipango
mingine. Spurs inataka kitita cha zaidi ya paundi milioni 35 kwa timu
yoyote ambayo inamhitaji kiungo wake huyo na Madrid bado wanaonekana
kujikung’uta mifukoni ili wapate kiasi hicho. Meneja wa Madrid Jose
Mourinho ameonyesha nia ya kumuuza Kaka mwenye miaka 30 kwenda Milan
ambako ndipo walipomnunua kwa paundi milioni 56 misimu miwili iliyopita
ili waweze kupata pesa za kumlipa Modric. Modric ambaye ana umri wa
miaka 26 raia wa Croatia anaonekana anaweza kucheza pamoja na Kaka
katika klabu hiyo lakini mshahara wa nyota huyo wa kimataifa wa Brazil
wa paundi milioni nane kwa mwaka ndio unaoonekana kuwa kikwazo kikubwa
kuhusiana na uhamisha huo.