OBAMA AIPONGEZA TIMU YA SOKA YA WANAWAKE KWA KUNYAKUWA DHAHABU.

Barack Obama.
RAIS wa marekani Barack Obama amekikpongeza kikosi cha timu ya taifa ya Marekani cha wanawake kwa kufanikiwa kunyakuw medali ya dhahabu katika michuano ya olimpiki jijini London kwa kuisambaratisha Japan kwa mabao 2-1 katika mchezo wa fainali uliochezwa katika Uwanja wa Wembley jana. Obama aliyasema hayo wakati alipotembelea kituo cha mazoezi cha olimpiki nchini humo kilichopo Magharibi mwa jimbo la Colorado kwa kuipongeza timu hiyo kwa kulipiza kisasi baada ya kupoteza mchezo wa fainali ya Kombe la Dunia dhidi ya Japan kwa changamoto ya mikwaju ya penati mwaka jana. Nyota wa mchezo huo alikuwa alikuwa Carli Lloyd ambaye alifunga mabao mawili katika mchezo huo yaliyoiwezesha timu yao kunyakuwa dhahabu ikiwa ni kama kifuta machozi baada ya mchezaji huyo kukosa mkwaju wa penati ambao uliipa Japan Kombe la Dunia mwaka jana. Timu ya soka ya wanawake ya Marekani imekuwa na mafanikio toka soka la wanawake liongezwe katika michuano ya olimpiki wakiwa tayari wameshinda michuano ya olimpiki ya mwaka 1996 iliyofanyika jijini Atlanta, Athens mwaka 2004 na Beijing mwaka 2008. Obama pia aliwapongeza wanamichezo wote ambao wameshiriki michuano ya olimpiki na olimpiki kwa walemavu mwaka huu jijini London kwa heshima kubwa waliloletea taifa hilo.