Mkalama-Singida
Oktoba 02, 2012.
Miradi......1
HALMASHAURI ya Wilaya Iramba Mkoani Singida imezitaka kamati za shule kubuni miradi itakayoziba pengo la fedha za ruzuku,zilizokuwa zinatolewa na Serikali.
Afisa elimu shule za msingi Wilaya Iramba, Leonard Ngaharo, alisema hayo kwenye mahafali ya tatu, kwa wanafunzi 30 wa shule ya msingi Darajani, iliyopo wilaya mpya ya Mkalama, mkoani Singida.
Alisema sababu kubwa ni wafadhili kujitoa na masharti magumu kutoka kwa wahisani, hali aliyowataka wananchi kubadilika kwa kamati za shule kubuni miradi itakayosaidia shule zote za msingi kujitegemea.
Mapema akitoa taarifa, mwalimu mkuu wa shule hiyo, Mary Ntoga alisema pamoja na changamoto zilizopo, lakini wazazi, walezi na wananchi kwa ujumla wanaoizunguka shule wanashiriki vema katika kuiendeleza shule yao.
Alisema kwa kuonyesha ushirikiano huo kwa vitendo, familia ya Daniel Kazimoto ya kijiji hicho inajitolea kila mwaka kulima bure shamba lenye ukubwa wa ekari 20 kwa kutumia jembe la kukokotwa kwa ng’ombe, huku shule ikiwajibika katika palizi pekee.