UOZO WA NORA WAANIKWA NA MUME WAKE.....

MUME wa mcheza filamu mahiri za Kibongo Nuru Nassoro ‘Nora’, Masoud Ally ‘Luqman’ ameamua kuvunja ukimya baada mkewe huyo kueleza sababu zilizofanya ndoa yao kuvunjika ambazo anadai siyo za kweli. Akizungumza na mwandishi wa habari hii, Luqman ambaye alitumia zaidi ya saa mbili kutoa ufafanuzi kuhusiana na  habari hiyo, alikanusha vikali kuwa wazazi wake ndiyo chanzo cha kufanya ndoa yao ivunjike.

Alisema kuwa mama yake alikuwa akimpenda sana Nora mpaka staa huyo alikiri kuwa mkwewe huyo anampenda, sasa anaumia kumsikia akidai ndoa yake ilivunjwa na wazazi wake.



Luqman alizidi kutiririka kuwa katika maisha yake ya ndoa aliyoishi na Nora, amewahi kuwa na furaha mara mbili tu kutokana na ugomvi wa kila siku ambao mara nyingi ulikuwa ukisababishwa na Nora.

“Kiukweli ndoa yangu nakumbuka imewahi kuwa na furaha mara mbili tu lakini kipindi chote ilikuwa ni ugomvi usioisha,” alisema.



Aliendelea kusema kuwa kutokana na ugomvi wa kila siku,  kuna siku Nora alishika kiwembe na kumchana nacho mkononi, hali iliyosababisha ashonwe nyuzi tano.

Alisema kuwa alikuwa akijitahidi kujishusha ili kuinusuru ndoa yake kwa sababu bado alikuwa akimpenda sana mke wake huyo lakini hakufanikiwa na kwamba siku nyingine Nora alimshikia kisu kisa kikiwa ni meseji ambayo hakuituma yeye.


Aliendelea kuweka wazi kuwa kutokana na migogoro ya hapa na pale, alishampa talaka zaidi ya mara mbili na kumrudia tena akidhani labda atajirekebisha na kuwa sawa lakini haikuwa hivyo.

“Hii talaka ya mwisho niliyotoa ilikuwa ni ya tatu  lakini yote hayo ni kwa sababu nilimpenda sana mke wangu,” alisema na kuongeza kuwa waliamua kuhamia Zanzibar ambapo Nora mwenyewe alikupenda.

Hata hivyo, walipofika huko bado aliendelea kumsumbua na alijaribu kumtishia kuwa kama ataendelea hivyo ataoa mke mwingine ambapo kauli hiyo ilimkera Nora na kuamua kurudi Dar.


Alisema aliporudi Dar, mara kwa mara alikuwa akimsihi arudi wakaendelee kuishi lakini Nora alikuwa akikataa na ndipo alipoamua kuoa mwanamke mwingine ambaye kwa hivi sasa tayari wamezaa naye mtoto mmoja.


“Nilikuwa nikijaribu sana kumbembeleza Nora arudi ili tuendelee kuishi lakini hakuwa tayari ndipo nilipoamua kuoa mke mwingine,” alimalizia Luqman.


SOURCE: GPL