UPDATE: MTANZANIA HUENDA AKAAGA BIG BROTHER AFRICA LEO


HATA kabla hawajamaliza kusalimiana, muongozaji wa kipindi cha Big Brother, IK alikuwa na habari mbaya kwa washiriki wa Tanzania na Zimbabwe.

Mara tu baada ya lango kuu kufunguliwa na wao kuingia ndani, IK aliwatangazia washiriki kuwa 'nomination' ingefanyika stejini wakati huo kwa kutumia staili mpya ya mashine tofauti na ile ya zamani ya kupendekezana wao kwa wao.


Baada ya kupewa taarifa hiyo mashine ililetwa jukwaani na kuzungushwa kisha kipira kimoja kiliruhusiwa kupita ambacho kingewataja washiriki walioingia kwenye mchakato wa kupigiwa kura na kutolewa hapo kesho.

Kwa bahati mbaya kipira kilichoandikwa Tanzania kilikuwa cha kwanza kutoka na hivyo kuwafanya washiriki wake, Hilda na Julio kuwa katika machakato wa kutolewa wiki hii. Hata hivyo biggie aliagiza kipira kingine kitolewe, Zimbabwe ilikuwa nchi ya pili kwa washirki wake kuingia kwenye mchakato wa kutolewa wiki hii.

Kitakachowawezesha Watanzania kubaki ni kura tu. unaweza kupiga kura kwa njia ya sms kwenda Vodacom  15726,
Tigo 15726, Zantel     15726  na Airtel 15726.


Unaweza pia kupiga kura mara nyingi kadri uwezavyo kwa njia ya mtandao ambao ni www.africamagic.tv/bigbrother.

Esperanca akubali kubaki
BAADA ya kutaka kumpa ugonjwa wa moyo mshiriki mwenzake Seydou, hatimaye Esperanca amekubali kubaki ndani ya shindano la Big Brother.

Haikuwa kazi rahisi kumshauri akubali kuendelea kubaki ndani ya shindano hilo, Seydou ambaye habari hiyo huenda ikawa ni mbaya kuliko zote alizowahi kusikia mwaka huu, alitumia kila mbinu kumshauri mwenzake abaki.

Seydou ilibidi atumie nguvu za ziada katika kumshauri kwa kuwa kuondoka kwa Esperanca kulimaanisha kuwa ni kuondoka kwake katika shindano hilo. Mlikuja wawili, mtaondoka wawili.

Goldie na Roki nao wakwaruzana
MASTAA katika jumba la Upville hawaishi kugombana kila kukicha, baada ya Barbz na Prezzo kukwaruzana, Goldie na Roki nao almanusura wazitwange.

Goldie alimrushia Roki midoli yake kutoka ndani ya koti huku akimfokea kwa madai kuwa amemkosea adabu.

Huku akitokwa machozi, Goldie alikuwa akirusha midoli huku akisema yuko tayari kuondoka katika jumba hilo wakati wowote kwa kuwa Roki hana adabu.

Prezzo na DKB walimchukua Goldie na kumtuliza, Roki alijaribu kuomba msamaha lakini wenzake hao walimwambia asubiri mpaka mwanamke huyo atakaponyamaza kabisa.

Downville washikana uchawi
WASHIRIKI katika jumba la Downville waanza kutuhumiana kuchezeana michezo michafu, wanawake hasa ndio wanaolalamikiana kuwa na uongo na kuchezeana rafu.

Hilda yeye anasema hana tofauti na mtu yoyote katika jumba hilo ila anashangaa kwanini wenzake wanamteta kila wanapokaa kwenye vikundi.

Wakiwa nje kila mmoja alianza kutoa dukuduku lake juu ya mshiriki anayehisi anamzungumzia vibaya wakati hayupo, hata hivyo kutokana na wingi wao hakuna suluhu iliyopatikana, mwishowe waliamua kumalizana kwa kunyamaza kimya na kucheza game ya 'never ever'.

Teclar ajipa umalkia
MSHIRIKI kutoka Zimbabwe, Teclar amejibatiza kuwa malkia wa ufalme wa Zamunda  nakuwateua viongozi mbalimbali huku mdogo wake ambaye ni mshiriki mwenza, Maneta akimteua kuwa msaidizi wake.

Amemteua mshiriki wa Afrika Kusini, Lee kuwa mtoto wa kiume wa mfalme, Luke wa Liberia amempa nafasi ya Uchungaji.

Teclar alimuomba Biggie ampe gauni la kimalkia lakini alimkatalia na kumtaka aendelee kutumia kila kilichopo ndani ya jumba hilo kufanikisha utawala wake.

Mshiriki huyo na kiongozi wa wiki hii, Keitta wamekuwa wakikwaruzana kwa kuwa hataki kufuata amri zinazotolewa akidai yeye ni malkia yupo juu yake.