PINDA: WAFICHUENI MAWAZIRI WAZEMBE


WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amewataka wananchi kuwafichua na kuwataja kwa majina mawaziri na watendaji wa serikali watakaozembea kwa kushindwa kusimamia vyema matumizi ya fedha za umma.


Pinda alisema hayo jana wakati wa sherehe za kuwasha Mwenge wa Uhuru zilizoenda sambamba na uzinduzi wa kampeni ya kitaifa ya sensa, zilizofanyika katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine, jijini Mbeya.

Alisema hakuna haja kwa wananchi kuangalia na kuwaacha mawaziri wanaharibu, badala yake wananchi wawashtaki hadharani mapema ili wachukuliwe hatua kabla hawajaliingiza taifa kwenye hatari.

Waziri Mkuu huyo alisema kuwa mabadiliko ya Baraza la Mawaziri yaliyofanyika yanatarajia kuleta utamaduni mpya wa matumizi ya fedha za umma na uwajibikaji zaidi.

“Tusisubiri wachache hao wanaoshindwa kusimamia fedha na mali za umma wakaendelea na tabia hizo, tuwaumbue na tuwataje mapema ili kurejesha nidhamu katika utendaji,” alisema Pinda.

Awali akizindua kampeni ya kitaifa ya sensa, Pinda alisema kuwa wameamua kufanya hivyo mapema ili kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kuhesabiwa katika zoezi la sensa ya watu na makazi linalotarajiwa kufanyika kuanzia Agosti 26 na kuendelea kwa mwaka huu nchi nzima.

Alisema sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 ina lengo la kupata takwimu kuhusiana na idadi ya watu na kukusanya taarifa za kina za kiuchumi, kijamii na maendeleo ya makazi.
Aidha aliwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi mbele ya tume ya kukusanya maoni ya Katiba mpya kutoa maoni yao yatakayotumika kuandikwa kwake.

Alisema tume hiyo iliyoteuliwa na Rais Kikwete Aprili 6, mwaka huu, hivi sasa inaendelea kujipanga kwa ajili ya kwenda mikoa yote nchini kwa lengo la kuanza kukusanya maoni ya wananchi kuhusiana na Katiba mpya.

Mwenge umeanza kukimbizwa rasmi jana mkoani Mbeya na kiongozi wa mbio za Mwenge Kitaifa Hornest Ernest Mwanosa.