Kaseja: Hawanifungi


EDO KUMWEMBE, ABDIDJAN
KIPA namba moja wa Taifa Stars, Juma Kaseja, ambaye pia ni nahodha wa timu hiyo, amesema wachezaji wa Taifa Stars wakitulia tu katika pambano la leo Jumamosi dhidi ya Tembo wa Ivory Coast, basi hawezi kuruhusu bao.


Akizungumza katika hoteli ya Ibis Plateau jijini hapa, Kaseja, anayeonekana kuipania mechi hiyo alisema mara nyingi kinachosababisha timu za Tanzania kufungwa mabao ya haraka haraka na timu za nje ni kutokana na kutotulia kwa wachezaji wake mechi inapoanza.
Nakwambia kaka kama wachezaji wetu wakitulia tu, hao akina Gervinho hawanifungi. Tatizo letu kubwa wakati mwingine ni kukosa utulivu. Nawaomba wachezaji wetu watulie tucheze mpira. Hakuna la ajabu sana litakalotokea kama tukitulia. Tatizo letu kubwa ni papara tu, aliongeza Kaseja.

Kaseja ambaye amecheza mechi kama hizi kwa muda mrefu tangu mwaka 2000 alipojiunga na Simba ya jijini akitokea Moro United ya Morogoro alikiri kwamba Ivory Coast ni maji mazito japo hawana hofu na timu hiyo. 

Kaka wao wapo 11 na sisi tupo 11, tunawaheshimu kwa sababu wanacheza timu kubwa barani Ulaya, lakini mimi nikitazama kikosi chetu naona tupo sawa. Tuna uwezo wa kufanya maajabu, alisema Kaseja.