MBOWE AMSHAMBULIA MKUCHIKA

MWENYEKITI wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, ametangaza vita na Mbunge wa Jimbo la Newala, John Mkuchika kwa kile alichodai ufisadi mkubwa anaowafanyia wakulima wa zao la korosho katika mikoa ya Lindi na Mtwara.


Mbowe akihutubia katika mikutano aliyofanya katika Kijiji cha Nanguruwe na Viwanja vya Mahakama vilivyopo Newala mjini, alisema atambana mbunge huyo pamoja na viongozi wengine wakati wa vikao vya Bunge katika mambo makuu matatu, ikiwemo Jeshi la Polisi, zao la korosho na ukusanyaji wa mapato.

Alisema Mkuchika ameshindwa kuwasaidia wananchi sambamba na umasikini mkubwa wanaokumbana nao katika jimbo lake, hivyo atahitaji majibu ya kueleweka, huku akiwata wasiwe na huruma tena kwa kuendelea kuikumbatia CCM, kwani imeshindwa kuwasaidia miaka mingi sasa.

Mbowe alisema licha ya jimbo hilo kuwa na utajiri mkubwa na uwezo wa kilimo cha korosho, mbunge huyo amewatenga, huku serikali yake ikichekelea kwa kuwatengenezea wananchi mfumo mbaya wa stakabadhi ghalani, ambao asilimia kubwa ni unyonyaji.

“Nawaambia ndugu zangu wa Newala, safari hii Waziri Mkuu Pinda na Mkuchika, lazima watanyooka tu, kwani tutawasha moto juu ya matatizo makubwa ya Lindi na Mtwara kwenye masuala ya upatikanaji wa madini ya gesi, mafuta, umasikini na juu ya mambo ya kilimo ikiwemo kuwateteeni juu ya zao la korosho,” alisema Mbowe.

Akemea siasa za dini
Mbowe pia aliwaasa wananchi wa Newala, kuepuka kugawanyika kwa misingi ya dini, kabila na utabaka ili kuliepusha taifa kuingia katika vita.

Alisema Serikali ya CCM imekuwa chanzo kikubwa katika kuchochea udini, kiasi cha kusababisha machafuko ya Zanzibar, kwa kuwaachia baadhi ya watu kufanya mihadhara ya kichochezi bila kuchukua hatua.
Tanzania daima