NAIBU WAZIRI WA FEDHA AZAMA SWALI LA MUUNGANO

WIZARA ya Fedha na Uchumi, imetangaza rasmi kumaliza mvutano wa siku nyingi ambao umesababisha malalamiko baina ya pande mbili za nchi, Tanzania Bara na Zanzibar, kuhusiana na utozaji kodi ya ushuru kwa bidhaa zinazotoka katika upande mmoja wa nchi.


Msimamo huo ulitolewa jana bungeni na Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi Saada Mkuya Salum, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Magogoni Hamad Ali Hamad (CUF), ambaye alitaka kujua ni kwa nini bidhaa hususan magari zinazotoka Zanzibar hutozwa tena ushuru katika bandari ya Dar es Salaam wakati mfumo wa ukusanyaji kodi (TRA) ni sawa.

Aidha, alisema inashangaza kuona bidhaa zinazotoka Tanzania Bara na kuingizwa Zanzibar hazitozwi ushuru.

Waziri huyo alikiri kuwa jambo hilo limeleta mgogoro wa muda mrefu baina ya wafanyabiashara wa pande hizo mbili na kwamba sasa Wizara ya Fedha imeamua sasa kukomesha kero hiyo.

“Mheshimiwa Spika, jambo hili limekuwa kero kubwa baina ya wafanyabiashara wetu na niseme waziwazi kuwa sasa kama alivyosema waziri wangu majuzi kule Zanzibar kwamba suala hili litapatiwa ufumbuzi wa kudumu na halitakuwepo tena,” alisema.

Aliongeza kuwa serikali itakaa pamoja na wafanyabiashara na wahusika wakubwa wa pande zote ili kuhakikisha wanatatua tatizo hilo ambalo ni la muda mrefu.

Awali katika swali la msingi mbunge huyo alitaka kujua kuna bandari ngapi hapa nchini ambazo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeweka watu kwa ajili ya kukusanya kodi na ni zipi.

Akijibu swali hilo hilo, Naibu Waziri, huyo alisema Mamlaka ya Mapato Tanzania imeweka watumishi wake katika bandari 21 ambazo zinapatikana katika nchi za jirani na ambazo biashara kati ya maeneo hayo yanafanyika kwa kuingiza au kutoa bidhaa nchini.

Alizitaja bandari hizo kuwa ni Dar es Salaam, Bagamoyo, Tanga, Pangani, Mtwara, Lindi, Kilwa Masoko, Msimbati, Zanzibar, Mkokotoni Zanzibar Wete Pemba na mkoani Pemba.

Nyingine ni Mwanza, Bukoba, Musoma, Kabwe, Kigoma Port, Kipili na Kasanga, Mbamba Bay na Ipyana- Kyela.