Zitto Kabwe Aiumbua Serikali


IMEDAIWA kuwa, serikali isingepaswa kuendelea kuomba msaada wowote wa fedha kutoka nje ya nchi, kama ingetekeleza mapendekezo ya bajeti ya kambi ya upinzani, yaliyotaka kupunguzwa kwa misamaha ya kodi kufikia asilimia moja ya pato la taifa, ambayo thamani yake ni sawa na fedha zote za misaada kutoka nchi wahisani.


Kauli hiyo, ilitolewa jana na Waziri Kivuli wa Fedha na Uchumi, Zitto Kabwe, ambaye aliweka wazi kuwa misamaha ya kodi ya asilimia tatu ya pato la taifa ni sawa na shs trilioni 1.03 ambazo ndizo zinazotolewa na nchi wafadhili kuisaidia Tanzania.

Zitto akitangaza mwelekeo wa bajeti yake kwa mwaka ujao wa fedha wa 2012/13, na kuainisha vipaumbele mbadala, alizidi kuianika serikali na kuitaka itoe maelezo ya kina ya kwa nini imeshindwa kutekeleza ahadi yake iliyoitoa bungeni, kwamba misamaha ya kodi itapunguzwa mpaka kufikia asilimia moja ya pato la taifa.

Zitto ambaye ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA) alisema kama serikali ingeyafanyia kazi mapendekezo ya kambi ya upinzani, yangewasaidia Watanzania kupunguza ukali wa maisha, na kuboresha maisha yao kwa kiwango kikubwa.

Alitaja mapendekezo yaliyopendekezwa na kambi ya upinzani, katika bajeti inayoisha, lakini yakawekwa kapuni na serikali kwa sababu zisizojulikana kuwa, mbali za misamaha ya kodi ni kupunguza kodi kwenye bidhaa za mafuta ya petroli na dizeli ili kushusha mfumuko wa bei.

Vipaumbele vingine vya kambi ya upinzani vilikuwa kufuta mfumo wa posho za vikao (Sitting allowances) na kupeleka sehemu ya tozo ya ujuzi (Skills Development levy-SDL) kwenye Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu.

Waziri huyo kivuli alisema ni mapendekezo mawili tu ya kodi za mafuta ya petroli na diseli na tozo ya SDL yaliyokubaliwa na kutekelezwa, wakati pendekezo la misamaha ya kodi lilikubaliwa, lakini serikali imeshindwa kulitekeleza, ikiwa ni pamoja na kukataliwa kwa pendekezo la kufutilia mbali posho za vikao, ambalo kambi ya upinzani imerejea wito wake wa kufutwa kwa mfumo wa posho za vikao (sitting allowances).