MADHARA YA FANGASI SEHEMU ZA SIRI....


Katika makala zetu ya maradhi ya ngozi tumeangalia maradhi ya ngozi yanayosababishwa na fangasi. Leo tuangalie fangasi wanaoshambulia sehemu za siri, yaani Tinea cruris. 

Fangasi wa maungo ya siri (Tinea cruris)
Aina hii ya fangasi ndiyo inayofahamika zaidi na  Watanzania wengi zaidi ya aina nyinginezo. Aina hii pia hutambulika kama muwasho wa aibu.

Dalili zake
Aina hii ya fangasi huambatana na dalili za aina nyingi, lakini kubwa kuliko zote ni kuwa fangasi hii huambatana na muwasho mkali wa eneo lenye maambukizi ya fangasi hawa.

Dalili nyingine zinazoonekana ni kama ifuatavyo:
-Rangi ya ngozi ya eneo lenye maambukizi hubadilika
-Huwa na muundo wa duara, mfano wa sarafu ya fedha.
-Ngozi kubanduka
-Ngozi hukauka
-Baada ya muda mrefu husababisha dalili nyingine zenye kuonekana kama kutoka kwa maji maji kwenye eneo la ngozi lililoathirika pamoja na kutoka kwa harufu mbaya kwenye eneo la ngozi lililoathiriwa.

Usambaaji wake
Kuna njia nyingi zinazoweza kusababisha uambukizi wa maradhi haya, lakini ili uambukizaji huu uwezekane lazima kuwa na mazingira rafiki ya kuwezesha fangasi kuishi na kuhama kwa urahisi.


Mazingira haya rafiki kwa kuruhusu fangasi hawa kuweza kutoka kwa mtu mmoja au sehemu moja ya mwili kwenda kwa mwingine huhitaji uwepo wa hali ya joto pamoja na majimaji (unyevunyevu).


Maradhi haya ni rahisi sana kuambukizwa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine kwa njia zifuatazo:

-Kugusana na mtu aliye na maambukizi tayari
-Kushirikiana kimapenzi na mwenza mwenye maambukizi hayo. 
-Kushirikiana mavazi na mtu aliyekwisha pata maambukizi
-Kushirikiana vifaa vya usafi wa mwili kwa mtu zaidi ya mmoja.

Ni nani yuko hatarini
Watu ambao huweza kupata maambukizi ya fangasi wa sehemu za siri ni wafuatao:
-Wale wanaofanya kazi zinazohusisha ukaaji kwenye maji yaliyotuama kwa muda mrefu;
-Watu wanaoshiriki mapenzi na wenza wenye maambukizi ya fangasi hao;
-Wale wanaotoka jasho sana hasa kwenye sehemu za mwili zilizojificha kama vile sehemu za siri;
-Wale ambao wana fangasi za kwenye vidole  kwani fangasi wale wanaweza kuhamishwa kupitia kwenye kucha na kuhamia kwenye eneo hilo la siri;
-Wanaofanya usafi wa mwili kwa kutumia maji yaliyobeba vimelea vya fangasi hao;
-Wasiojikausha vizuri maungo ya sehemu za siri;
-Watu wenye maradhi yanayosababisha kushuka kwa kinga, hususan kisukari ;
-Watu wanaovaa nguo zaidi ya moja hali inayosababisha mwili kushindwa kupunguza joto lake hivyo kutoa jasho;
-Watu wanaovaa nguo za kubana sana hasa zile zinazobana sana kwenye maeneo ya maungo ya siri;
-Watu wenye unene wa kupindukia;
-Wale wanaokunywa dawa za kuua vimelea (antibiotics) kwa muda mrefu;
-Wenye ujauzito (ujauzito huchangia kushuka kwa kinga ya mwili).
Itaendelea....
 Mwananchi