WAHESHIMIWA MADIWANI,
CCM NA TLP
HALMASHAURI YA MANISPAA YA ARUSHA
YAH: MGOGORO WA MEYA ARUSHA MJINI
Tafadhali husika na kichwa cha habari hapo juu.
Sisi
Madiwani wa CHADEMA tumefikiri na kutafakari kwa kina kuhusu
mustakabali wa maendeleo ya wananchi wa Manispaa ya Arusha Mjini. Kwa
nafasi yetu ya wawakilishi na utetezi wa wananchi Arusha kwa umoja wetu
ni vema tufikiri na tutafakari kwa kina kwa pamoja hasa kipaumebele
ikiwa ni kutanguliza HAKI na MAENDELEO katika kumlenga kila mkazi wa
aliyepo katika Halmashauri yetu. NI vema tukawa WAKWELI na WAZELENDO kwa
wananchi wetu wa Arusha, huku wote tukijua kwa kina kile kilichotokea
Arusha.
Kwa
muda mrefu kumekuwa na mgogoro wa Uchaguzi wa MEYA wa manispaa ya
Arusha, ambayo ilitokana na ukiukwaji wa kanuni na taratibu za uchaguzi
wa Meya ambayo akidi yake ilikuwa haijatimia. Ikumbukwe kuwa Mhe. Kivuyo
ambaye katika sakata hilo alijikuta akichaguliwa kwa hila kuwa NAIBU
MEYA, alifikia hatua ya kujizulu nafasi hiyi na kukiri mbele ya
waandishi wa habari na wananchi wa Arusha kuwa uchaguzi uliofanyika
haukuwa wa haki na yeye alipewa nafasi hiyo kwa hila, kitu ambacho baada
ya tafakari ya kina aliamua kujiuzulu ili asiwe sehemu ya dhambi hiyo
na kujikuta anakalia KITI CHA DAMU. Jambo hili pia limekuwa likisemwa na
baadhi ya madiwani wa CHAMA CHA MAPINDUZI pindi tunapokutana nao kuwa
mfumo wa chama cha CCM unazuia kuyatamka haya lakini ukweli ni kuwa huo
uchaguzi wa meya uliofanyika na Mhe Gaudence Lyimo kupata nafasi hiyo
ulikuwa batili kwa mujibu wa kanuni, lakini mbaya zaidi, umepelekea damu
kumwagika, jambo ambalo ndio baya.
Wote
tunashuhudia jinsi ambavyo mgogoro huu ulivyo na madhara makubwa sana
kwa wananchi wetu na sisi pia ambao ni sehemu ya jamii hiyo hiyo. Mbali
na kusababisha watu watatu kupoteza maisha, pameendelea kutokea
sintofahamu kubwa kutoka kwa wananchi jambo ambalo limeendelea kuzidisha
hasira kwa wananchi kwa serikali. Jambo hili ni vema likafanyiwa kipimo
maana mchezo huu na hila hii inaweza kuzaa balaa ambalo sio rahisi
kulimudu tena.
Dharau
na makusudi yanayofanywa na chama cha mapinduzi, mathalani Mhe Gaudence
Lyimo na MKURUGENZI wa halmashauri katika kupuuzia wito wa CHADEMA kuwa
HAKI haikutendeka, KANUNI zilivunjwa na hivyo uchaguzi wa MEYA ufanyike
upya kwa kufuata kanuni sasa inafika mahali haivumiliki na hapo ndipo
itakuwa mikononi mwa wananchi na sio CHADEMA tena.
Sambamba
na hali hii, pia mgogoro huu unatumiwa na watendaji wa Halmashauri
kufanya mambo yao yasiyo ya kiuadilifu kwani hakuna udhibiti wa kabisa
katika uendeshaji wa halmashauri yetu. Waheshimiwa madiwani, katika
ukweli huu, MKURUGENZI na huyo anayeitwa MEYA watatoa wapi ujasiri na
kujiamini “moral authority” ili hali wao wameshiriki dhambi mbaya ya
kuchakachua kanuni za kufanya uchaguzi wa meya isivyo halali na mbaya
zaidi Mhe Gaudence kuendelea kung’ang’ania nafasi hiyo kwa kiwango cha
damu ya watu kumwagika bila hata kujali??
Hata
hivyo, hata kama Mhe Gaudence Lyimo hatajali wito huu ambao kwetu ni
wito wa mwisho kwake na chama chake, jambo hili tunaliacha kwa MUNGU
mwenye HAKI atashughulika nae kwa wakati wake na muda si mrefu tutapata
majibu ya maombi yetu. Pili tunaliacha jambo hili kwa wananchi ili
waamue kwa sababu wameshajua wazi kuwa Mhe Gaudence Lyimo na chama chake
waliamua na wameendelea kuwafanyia uhuni katika mji wao. Sisi
tumeliacha kwao waamue watakavyoamua.
Tunafahamu
kabisa katika nafsi na mioyo yenu mnafahamu uchaguzi haukuwa halali
lakini mnashindwa kusimamia ukweli kwa sababu ya ubinafsi na kukosa
uzalendo kwa wananchi wa Arusha kwa kutanguliza maslahi yenu mbele, kitu
ambacho tusingependa kipewe tafsiri hiyo
Tunawasihi
kwa dhati kabisa tuamue kwa pamoja kwa manufaa ya Arusha tukubaliane
kama viongozi wazalendo, wapenda maendeleo na wenye hofu ya MUNGU
tufanye uchaguzi wa MEYA wa Halmashauri ya Arusha ambao utakuwa ni
halali kwa vyama vyote.
Nchi
nyingi za Afrika kumekuwa na vita vya wao kwa kwao kwa sababu ya uchu
wa madaraka. Hili limetokea pia hapa Arusha watu wamekufa kwa sababu ya
MEYA, hii ni aibu na ni dhambi kwa kung’ang’ania madaraka ambayo si
haki.
Waheshimiwa
madiwani wenzetu hata juhudi za serikali kufanya maendeleo wananchi
wengi wa Arusha bado hawana imani na serikali yao kwa sababu ya MEYA tu.
Hivi sasa kuna mradi wa ujenzi w barabara unaondelea ukweli ni kwamba
jambo hili ni zuri lakini wananchi wanalibeza sana kama vile linafanywa
kwa hila. Kwa nini iwe hivi??
Kimsingi
tunataka MEYA ambaye yupo huru kutembelea kata zote kwa ajili ya
maendeleo bila kujali itikadi ya chama chake. Hatutaki MEYA anayevizia
misiba na harambee.
Mwisho
tunamwomba Mh. Gaudence Lymo atafakari kwa kina kwa kumuomba MUNGU wake
ampe hekima na ujasiri wa kuchukua maamuzi magumu ya kujiuzulu nafasi
ya UMEYA na uchaguzi wa kidemokrasia ufanyike kwani utampa heshima na
amani katika maisha yake yote.
Tunaomba
Waheshimiwa Madiwani wenzetu kwa pamoja tuseme dhambi hii imetosha na
tutubu kwa kufanya uchaguzi wa haki na Amani. Na kwa dhati kabisa yeyote
atakayechaguliwa hata kama ni Mh. Gaudence tutampa ushirikiano wa dhati
kabisa.
Tunaomba
ushirikiano wenu katika jambo hili ambalo ni la msingi kwa maendeleo ya
watu Arusha. Kila mmoja kwa imani yake aombee jambo hili kwani halitaki
ushabiki linahitaji utulivu wa akili.
WAHESHIMIWA
MADIWANI, FANYENI TAFAKARI YA KINA, ZINGATIENI JINSI WANANCHI KATIKA
KATA ZENU WANAVYOWATAZAMA, ni matumaini yetu kuwa tutafanya uchaguzi wa
MEYA ndipo tufanye uchaguzi wa Naibu MEYA. Na jambo hili litakuwa ni
ushindi na sifa iliyotukuka kwa MADIWANI WOTE na sio kundi fulani la
watu.
Asanteni sana
Doita Isaya Harri
Mwenyekiti madiwani wa CHADEMA
Nakala:
Katibu wa CHADEMA (M)
Katibu wa CCM (M)
Katibu wa TLP (M)
Mkurugenzi wa Halmashauri – Arusha Mjini