Kigoma All Stars wanastahili kupongezwa

'Una la kuongeza'Huu ni mwaka ambao mkoa wa Kigoma utaongelewa sana kwenye burudani. Hongera nyingi ziende kwa yule aliyekuja na wazo hili lenye thamani ambalo limeunyanyua mkoa wa Kigoma katika kipindi kifupi mno.
Tangu itoke Leka Dutigite, Kigoma imejipatia sifa kubwa kwa kujulikana miongoni mwa wasanii waliojuu kwenye muziki wa kizazi kipya nchini kuwa wanatokea huko.
Ukizungumzia Diamond Platnumz na ukaona jinsi kijana alivyofanikiwa mpaka kupiga show Big Brother, ni halali uheshimu mkoa ulio asili yake, Kigoma. Tunafahamu kimaendeleo Kigoma ni miongoni mwa mikoa iliyonyuma kwa Tanzania. Wanapaita ‘Kigoma mwisho wa reli’. Jitihada hizi za mbunge wa Kigoma kaskazini, Mheshima Zitto Kabwe kuwapa support wasanii wenye asili ya Kigoma, sasa zimegeuka mfano wa kuigwa.
Tangu wimbo ‘Leka Dutigite’, neno la kiha lenye maana ya Acha Tujidai, Kigoma umekuwa ni mkoa unaojadiliwa sana na wapenzi wa burudani mitaani na kwenye mitandao ya kijamii. Na hapo ndo utakapogundua kuwa Tanzania hakuna ukabila. Watu wa mikoa mingine wameupenda wimbo huu na kuwapongeza wasanii hao.
Ni wimbo uliofanywa na masupastaa haswaa wa Tanzania. Diamond, Peter Msechu,Ommy Dimpoz, Baba Levo, Banana Zorro, Chege, Mwasiti, Linex, Queen Darling, Rachel na wengine wasanii waliojuu sana nchini. Ni movement ambayo ikiwa nyuma ya mbunge mwenye kipaji cha uongozi, Mhe. Zitto, inayoweza kuleta mabadiliko makubwa kwenye mkoa huo, kiuchumi na kisiasa.
Ni muungano unaoweza kupeleka maendeleo makubwa kwa kutumia mwavuli wa burudani. Ni movement ambayo itawaamsha wasanii wengine na hata watu wa kawaida kuthamini asili yao. Wanasema mtu asiyekuwa na kwao ni sawa na mtumwa. Itawaamsha wasanii waliopo Dar es Salaamn(kitovu cha tasnia ya burudani nchini) kujivunia mkoa ama hata kijiji anachotokea. Chema vizuri kuigwa.
Mikoa mingine haitakuwa na hasara ikifanya hivyo pia. Uzuri wa muungano kama huu, huchangia kukua kwa sanaa kwenye mkoa husika. Tangu Leka Dutigite itoke, kuna wasanii wengi wachanga wa mkoani Kigoma waliopata morali ya kuongeza juhudi zaidi kimuziki ili wafanikiwe na hatimaye kupewa heshima kama hiyo ya kujiunga na wakali wa mkoa huo. Japo baadhi yao kama wanavyosema kuwa Kigoma ni asili yao tu lakini hawakukulia huko, asili ipo pale pale na ni jambo la msingi kuutangaza.
Baada ya kitendo hicho, leo hii watu wengi wametamani wasanii wa mikoa yao wafanye kitu kama hicho pia. Huo ni wivu wa maendeleo kama asemavyo Monty Khatau Ezel, “Nimevutiwa na hiyo kitu, natamani ningekuwa natokea Kigoma,nina ugonjwa wa wivu wa maendeleo,najivunia kutokea kusini,LINDI wajiandae mafanikio yanawajia.”
Ibrahim Athumani Masokola naye anasema, “Nahisi katika mambo ya kuiga kwa baadhi ya watu kama waheshimiwa ni pamoja na hili analofanya mhe Zitto kwani ni njia mojawapo ya kuwafikia wananchi kwa urahisi HONGERENI SANA WOTE mlohusika kwa namna moja au nyingine.”
Naye Zulu Agrey Mnkeni anasema, “Natamani nami ningekuwa wa KIGOMA ila ndo bahati mbaya natoka KILIMANJARO naogopa kuitwa MKABILA.”
Kitendo hicho cha Mheshimiwa Zitto kuungana na wasanii ili kuutangaza mkoa wa Kigoma,kinamweka karibu zaidi na vijana waliowengi nchini na kumsafishia njia yake kwa mambo makubwa zaidi katika career yake kama mwanasiasa. Hongereni Kigoma All Stars!

Photos by: Pernille Bærendtsen