Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA)Kuzindua Kampeni Maalum Kwa Ajili ya Ujenzi wa Hosteli za Wanafunzi wa Kike Katika Shule za Sekondari Nchini

 Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), Esther Abayo akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuhusu uzinduzi wa kampeni maalum kwa ajili ya ujenzi wa hosteli za wanafunzi wa kike katika Shule za Sekondari nchini utakaofanyika tarehe 14 Julai Kibaigwa mkoani Dodoma. Kushoto ni Meneja Habari Elimu na Mawasiliano, Sylvia Lupembe. 
  Meneja Habari Elimu na Mawasiliano wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), Sylvia Lupembe akifafanua jambo kuhusu uzinduzi wa kampeni maalum kwa ajili ya ujenzi wa hosteli za wanafunzi wa kike katika Shule za Sekondari nchini utakaofanyika tarehe 14 Julai Kibaigwa mkoani Dodoma. Katikati ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), Esther Abayo na Mkurugenzi wa Uhamasishaji Rasilimali Watu, Seif Mohamed.
 Mkurugenzi wa Uhamasishaji Rasilimali Watu, Seif Mohamed akifafanua jambo kuhusu  uzinduzi wa kampeni maalum kwa ajili ya ujenzi wa hosteli za wanafunzi wa kike katika Shule za Sekondari nchini utakaofanyika tarehe 14 Julai Kibaigwa mkoani Dodoma. Katikati ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), Esther Abayo.
--
 
Mamlaka ya Elimu Tanzania inatarajia kuzindua kampeni kwa ajili ya ujenzi wa hosteli za wanafunzi wa kike katika shule za sekondari nchini tarehe 14 Julai 2012.
Uzinduzi huu utafanyika mkoani Dodoma katika mji mdogo wa Kibaigwa ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Mh. Philip Mulugo(Mb). Pia uzinduzi huu utahusisha viongozi mbalimbali wa serikali, wabunge, Wadau wa elimu, wakazi wa eneo hilo, wazazi na wanafunzi wa shule ya sekondari Kibaigwa na zingine zilizo jirani.
Katika Kampeni hii Mamlaka inalenga kujenga hosteli 30 kupitia michango ya wadau mbalimbali. Kiasi kinacholengwa ni shilingi za kiatanzania 2.3 bilioni ambapo kila bweni litagharim shilingi millioni 78 bila samani. Jumla ya wanafunzi wa kike 1,504 watahudumiwa pindi ujenzi wa hosteli hizi utakapokamilika.
Shule za sekondari zitakazofaidika na mradi huu ni Ufana - Manyara, Mibukwe - Tanga, Kibaigwa - Dodoma, Milola - Lindi, Nyihara - Mara, Lundo - Ruvuma, Butundwe - Mwanza na Buseko hill – Kigoma.
Serikali kupitia Mpango wa Maendeleo ya Elimu inakusudia kujenga hosteli 100 katika maeneo mbalimbali nchini kwa ajili ya wanafunzi wa kike 4,800 ifikapo mwaka 2015. Kutokana na wingi wa shule za sekondari nchini na ongezeko la mahitaji ya hosteli ndipo Mamlaka ikaamua kuongeza nguvu juhudi hizo kwa kushirikisha jamii kuchangia fedha na rasilimali nyingine ili kujenga hosteli hizo 30 ambazo ni asilimia 30 ya azimio la serikali.
Dhamira ya Mamlaka ya Elimu Tanzania kujikita katika suala la hosteli kwa wanafunzi wasichana wa sekondari ipo katika mpango mkakati wake (ROLLING CORPORATE STRATEGIC PLAN 2010/11 – 2014/15) ambapo kwa awamu ya kwanza imedhamiria kujenga hosteli 30.
Changamoto za ukasefu wa hosteli kwa wanafunzi wa kike wanaotokea nyumbani au waliopanga ni pamoja na muda mchache wa kujisomea kwani wanalazimika kutimiza majukumu ya nyumbani kabla ya kuanza kujisomea, vishawishi na udhalilishaji wakiwa njiani wakielekea shuleni, wale waliopanga nyumba za karibu na shule wanajikuta wakitumia muda mwingi kutafuta maji na chakula na pia wanajikuta wakiwa katika ushawishi mkubwa wa kuingia katika mapenzi wakiwa na umri mdogo, hali inayopelekea kupata mimba na hivyo kukatisha masomo
Takwimu za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi .(MoEVET Best, 2011) zinaonesha wanafunzi wa kike 16,656 walifukuzwa shule kutokana na mimba kati ya mwaka 2008 na 2010.  Wakuu wa shule wamashauri kwamba tatizo hilo linaweza kupunguzwa iwapo wanafunzi wa kike watapatiwa makazi bora na salama katika maeneo ya shule.
Tunawaomba wadau wa Elimu na watanzania kwa ujumla kuchangia katika  kampeni hii kwa fedha taslimu au vifaa kama vifaa vya ujenzi au samani za hosteli. Kwa michango ya fedha taslimu unaweza kuchangia kwa kutuma fedha katika akaunti ya Mfuko iliyopo benki ya CRDB 01J1027639900, au kwa kupitia akaunti ya M-pesa namba 404040 Unaweza pia kuwasilisha mchango wako katika ofisi za Mamlaka ya Elimu Tanzania zilizopo Mikocheni barabara ya kambarage au katika vituo vya televisheni vya ITV, channel ten na star TV