MODRIC AOMBA RADHI KWA KUKOMA KUSAFIRI NA TIMU.

KIUNGO wa kimataifa wa Croatia na klabu ya Tottenham Hotspurs Luka Modric ameomba radhi kwa mwenyekiti wa klabu hiyo Daniel Levy kwa kufanya mgomo na kushindwa kusafiri na wenzake katika ziara Marekani. Kiungo huyo alipita katika makao makuu wa klabu hiyo kumuomba radhi Levy kutokana na tukio hilo kabla ya kupanda ndege kwenda kujiunga na wenzake waliopo katika ziara nchini Marekani kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa Ligi Kuu nchini Uingereza. Modric ambaye ana umri wa miaka 26 alitegemea mgomo aliofanya wa kukataa kusafiri na timu katika uwanja wa ndege wa Heathrow juzi itasaidia kutoa msukumo wa kukamilika kwa mchakato wa kumuuza katika timu ya Real Madrid. Lakini mbinu hiyo ilionekana kumkera Levy ambaye alitaka kumtoza faini ya paundi 15,000 katika kila siku ambayo atakuwa akiendelea na mgomo huo. Naye meneja wa Spurs Andre Villas-Boas ameonyesha kukerwa na kitendo hicho na kusema kuwa hakutegemea kufanywa na mchezaji mwenye hadhi kama ya Modric lakini anategemea suala hilo limalizika haraka ili waweze kuendelea na maandalizi ya msimu mpya wa ligi.