Tamko la HakiElimu kuhusu Mgomo wa Walimu Tanzania, Agosti 2012

Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu, Bi. Elizabeth Missokia (kulia) akitoa tamko kwa wanahabari kuhusiana na mgomo mchana huu jijini Dar es Salaam. Wa pili kutoka kulia ni Meneja wa Kitengo cha Habari na Ushauri, HakiElimu. (Picha na Joachim Mushi)

CHAMA Cha Walimu Tanzania (CWT) kiliitisha mgomo kwa walimu wote nchini kuanzia Jumatatu tarehe 30 Julai 2012 mpaka kitakapowajulisha vinginevyo. CWT kinaona mgomo ndio njia sahihi itakayoishinikiza Serikali kutekeleza madai ya walimu na kuwaboreshea mazingira ya kazi walimu. Mgomo huu leo unafikisha siku ya nne mfululizo.

HakiElimu inatambua kuwa walimu wamekuwa na mgomo baridi kwa muda mrefu sasa. Utafiti uliofanywa na HakiElimu mwaka jana ulibaini kuwa asilimia 40.6 tu ya walimu katika sampuli ya utafiti ndio walioonesha nia ya kuendelea kuwa walimu, wakisema mazingira magumu na maslahi duni ndio sababu kubwa za kuwavunja moyo. 

Uthibitisho mwingine wa kuwepo kwa mgomo baridi unatokana na kushuka kwa ufaulu wa wanafunzi katika mitihani ya Taifa. Kwa mfano katika shule za msingi, takribani nusu ya wanafunzi wamekuwa hawafaulu kwa miaka 3 sasa; huku mwaka 2011 pekee ukiwa na asilimia 46.5 ya watahiniwa waliofeli mitihani yao ya darasa la saba; na kwa sekondari wanafunzi takribani asilimia 90 walipata daraja la nne na sifuri.

Hali hii pia inadhihirishwa zaidi na uwepo wa wanafunzi zaidi ya 5,000 mwaka huu nchini walioandikishwa kujiunga na masomo ya sekondari kutokujua kusoma na kuandika.

Pia ripoti ya utafiti uliofanywa kwa niaba ya African Economic Research Consortium na Benki ya Dunia mwaka 2011 inaonesha kwamba walimu wa shule za msingi Tanzania wanafundisha kwa wastani wa masaa mawili na dakika nne tu kwa siku; kati ya masaa 5 na dakika 12 yaliyo katika ratiba ya siku moja.

Mambo haya yote yanadhihirisha kuwa mgomo baridi wa walimu umeendelea kuwepo, na kuwaathiri zaidi wanafunzi. Wanafunzi hawawezi kujifunza bila walimu; na walimu bila kufundisha kwa moyo, wanafunzi hawawezi kujifunza kwa ukamilifu.

Ni dhahiri kuwa mgomo huu wa walimu umekuwa na madhara makubwa kwa wanafunzi na jamii kwa ujumla. Wanafunzi wanakosa masomo. Hii itachelewesha kumaliza ‘mihtasari’ (syllabuses) ya kufundishia, na kuwaumiza zaidi wale watakaofanya mitihani yao ya Taifa mwaka huu. 

Usalama wa wanafunzi uko hatarini, hasa wanapoamua kwenda shuleni kwa kuhisi kuwa huenda walimu wao watafundisha kwa siku hiyo. Ni hatari sana wanafunzi kuwepo shuleni bila walimu. Wanakosa mwongozo wa walimu, na kuishia kurandaranda maeneo ya shule, ama mitaani.

Pia mgomo huu unajenga mtazamo hasi wa jamii kuhusu kazi ya ualimu. Wanafunzi na wazazi wao wanaendelea kutengeneza tafsiri kuwa kazi ya ualimu ni duni sana, na baadhi ya kauli za serikali kuhusu mgomo huu haziijengei hadhi kazi hii adhimu. HakiElimu pia inaamini kuwa mgomo huu utaligharimu Taifa kwa namna mbalimbali. 

Kwa kadri unavyochelewa kwisha, unaweza kubadilisha mihula masomo, ratiba za mitihani ya Taifa, na hata sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika mwezi huu inaweza kuingia dosari. Wazazi wa wanafunzi hasa walio shule za bweni wanatafakari hatma ya watoto wao. Je, wawarudishe nyumbani au waendelee kukaa shuleni?
Baadhi ya wanahabari waliusikiliza uongozi wa HakiElimu
Baada ya kuyatafakari haya, HakiElimu inapendekeza yafuatayo:

1. Kila mwanafunzi ana haki ya kujifunza na kuelimishwa. Hivyo basi, Serikali na Chama Cha Walimu Tanzania wanapaswa kufikia makubaliano haraka kadri inavyowezekana, kwa kuwa waathirika wakubwa wa mgomo sio wao wenyewe, ni wanafunzi.

2. Mgomo huu ushughulikiwe na uishe kabisa. Usiishie kuwaona walimu wamerejea kufundisha, huku wakiwa na kinyongo. Hii italeta mazingira ya kuendeleza mgomo baridi; na madhara yake ni makubwa zaidi.

3. HakiElimu inawakumbusha walimu kuwajibika. Wadai haki zao, huku wakitimiza wajibu wao wa kufundisha na kuendeleza elimu yetu. Wafundishe kwa bidii bila kinyongo, kwa kuwa wasipowajibika watakuwa wanawaumiza wanafunzi na jamii kwa ujumla. Mgogoro uliopo ni baina yao na Serikali, na si wanafunzi.

4. Kusema serikali haina uwezo wa kuboresha maslahi na mazingira ya kazi ya watumishi wake; haileti unafuu wa maisha kwa watumishi wa umma. Gharama za maisha zinazidi kupanda, na mfumuko wa bei nao unawaumiza watumishi kila siku. Hivyo, Serikali itafute vyanzo mbadala vya mapato. Isitoshe, serikali iweke malengo, mipango na mikakati ya kuboresha elimu na mazingira ya kufundishia kwa kuwa ndio njia muafaka na ya haraka ya kuiletea nchi maendeleo.

5. HakiElimu inasisitiza kwamba nchi itafanikiwa kuboresha elimu endapo tu itawekeza kwa walimu kwa kuboresha mazingira ya kazi, maslahi ya walimu, kuwashirikisha walimu katika maamuzi kuhusu masuala ya elimu na kuwapa walimu mafunzo kazini. Elimu bora haiwezi kuletwa na walimu walio hoi!

6. Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania litenge muda kujadili suala hili kwa kina na kuishauri serikali, hasa kuhusu tahadhari za kuchukua ili tatizo kama hili lisitokee tena. Bunge lina wajibu wa kuishauri na kuisimamia Serikali kuhusu sera, utendaji na usimamizi wa elimu nchini. 

Inasikitisha kwamba Bunge linakwepa kujadili tatizo hili kwa maelezo kwamba liko mahakamani. Tunaamini kwamba mahakama italiangalia suala hili na kutenda haki, lakini wajibu wa Bunge uko pale pale.

7. Viongozi wa Serikali wasiwabeze walimu; kwa kufanya hivyo wanawakatisha tamaa. Hata kama baadhi ya walimu hawakusoma kwa miaka mingi kama ilivyo kwa fani nyingine, wana umuhimu mkubwa sana. Ndio wanaowaandaa watanzania wa leo na kesho kimtazamo na kimaarifa. Hivyo, kudai kuboreshewa mazingira ya kazi ni haki yao; na Serikali inaweza kutimiza wajibu wake kwa kuwasikiliza na kushauriana nao bila ubabe na kejeli.

8. Serikali ijijengee utaratibu wa kuboresha mazingira ya watumishi wake, na si kusubiri kwenda mahakamani kuzuia watumishi kugoma. Watumishi wa umma watafanya kazi kwa ari endapo tu wameridhika na mazingira ya kazi na maslahi yao; na si kwa kutumia uamuzi wa mahakama peke yake. 

HakiElimu ni shirika la jamii linalowawezesha wananchi kubadilisha elimu, ndani na nje ya shule; kuathiri utungaji na utekelezaji madhubuti wa sera; kuchochea majadiliano ya umma na mabadiliko ya kijamii yenye ubunifu; kufanya utafiti, uchambuzi na uhamasishaji wa sera, na kushirikiana na wabia ili kuendeleza ushiriki, uwajibikaji, uwazi na haki za jamii. Shirika linataka kuona Tanzania inaongeza uwazi, haki na demokrasia kwa kuwapa watu wote fursa ya kupata elimu inayochochea usawa,ubunifu na fikra tunduizi.
Elizabeth Missokia Mkurugenzi Mtendaji