Hakimu Aburutwa Kortini Kwa Rushwa


Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Ilala Pamela Kalala (kushoto),akitoka katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam jana,baada ya kusomewa shitaka la kuomba rushwa ya Shilingi milioni tatu. HAKIMU Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Ilala, Pamela Kalala amepandishwa kizimbani kwa tuhuma za kuomba na kupokea rushwa kutoka kwa mke wa mmoja wa washtakiwa aliokuwa akisikiliza kesi yao.  Hakimu Kalala alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana asubuhi na kusomewa mashtaka matatu ya kuomba rushwa ya Sh3 milioni na kupokea rushwa ya Sh900,000 kwa nyakati tofauti. Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Allen Kasamala alidai mbele ya Hakimu Mkazi, Aloyce Katemana kuwa mshtakiwa alitenda makosa hayo kwa nyakati tofauti Februari, mwaka huu.
 Katika kosa la kwanza, Kasamala alidai kuwa mshtakiwa huyo aliomba rushwa ya Sh3 milioni kutoka kwa Josephine Omar ambaye ni mke wa mmoja wa washtakiwa katika kesi namba 703 ya mwaka 2008 inayohusu kujipatia fedha kwa njia zisizo halali. Kasamala alidai kuwa mshtakiwa alimwomba Josephine kiasi hicho cha rushwa ili kumshawishi ampendelee mumewe katika kutoa uamuzi wa kesi hiyo aliyokuwa akiisikiliza. Katika shtaka la pili, Kasamala alidai kuwa Februari, tarehe isiyofahamika, mshtakiwa alipokea rushwa ya Sh800,000 kutoka kwa Josephine na katika kosa la tatu, alidai kuwa Februari 6, mwaka huu mshtakiwa alipokea rushwa ya Sh100,000 kutoka kwa mwanamke huyo. Kasamala alidai kuwa mshtakiwa alitenda makosa hayo akiwa mwajiriwa wa Idara ya Mahakama kwa wadhifa wa Hakimu Mkazi. Alisema Kalala alitenda makosa hayo kinyume cha Kifungu cha 15 cha Sheria ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007. 


Hata hivyo, mshtakiwa alikana mashtaka yote na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika. Hakimu Katemana alimwachia mtuhumiwa huyo kwa dhamana, baada ya kutimiza masharti ambayo ni pamoja na kusaini bondi ya Sh1 milioni na kuwa na mdhamini mmoja anayefanya kazi katika taasisi inayotambulika, ambaye pia alisaini bondi ya Sh1 milioni. Hakimu Katemana aliahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 23, kwa ajili ya kutajwa. Mahakimu na rushwa Kalala anakuwa hakimu wa nne kupandishwa kizimbani katika Mahakama ya Kisutu kwa tuhuma za rushwa, katika kipindi cha miaka mitano. 


Desemba mwaka 2007, aliyekuwa Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Temeke, Jamila Nzota alipandishwa kizimbani katika Mahakama hiyo akituhumiwa kupokea rushwa ya Sh700,000. Nzota alikuwa akikabiliwa na tuhuma za kuomba rushwa hiyo kutoka kwa Mollel, aliyekuwa Mwakilishi wa Kampuni ya Amanarth Enterprises Ltd iliyokuwa na kesi ya madai namba 33/207 mbele yake, ili amsaidie. Katika kesi hiyo, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu, Hanzron Mwankenja (mstaafu kwa sasa), alimhukumu Nzota kwenda jela miaka kumi na moja kuanzia Mei 22, 2009, baada ya kupatikana na hatia katika makosa manne yaliyokuwa yakimkabili. Hata hivyo, Hakimu Mwankenja alisema mshtakiwa atatumikia adhabu zote kwa pamoja, hivyo alitumikia kifungo cha miaka mitatu jela. Nzota hakuridhika na hukumu hiyo na kupitia kwa Wakili wake, Majura Magafu alikata rufaa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, lakini katika hukumu iliyotolewa na Jaji Emilian Mushi, Aprili 30, 2010, alishindwa tena. Wengine ni aliyekuwa Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Adolf Mahai, (2007) na Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Ukonga, Ndovela Kihenga, "http://www.mwananchi.co.tz/habari">http://www.mwanan