ADAI WATEULE WAPYA WANA TASWIRA YA UFISADI
KATIBU Mkuu
wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa,
ameichambua safu mpya ya uongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) iliyoundwa
hivi karibuni mjini Dodoma, akisema wana taswira ya ufisadi.
Amesema kuwa hali hiyo inatokana na baadhi yao kuhusika kwenye matukio kadhaa ya kifisadi moja kwa moja.
Akizungumza
na Tanzania Daima jana kuhusu mtazamo wake kwa safu hiyo mpya ya uongozi
wa CCM iliyoundwa na Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete, katika
mkutano mkuu uliomalizika juzi, Dk. Slaa alisema haoni jambo jipya.
“Nadhani hakuna jambo jipya, kipya ni kwamba wameteuliwa jana, lakini wote ni wazoefu wachafu,” alisema.
Katika safu
hiyo, Kikwete anasaidiwa na makamu wawili, Philip Mangula wa bara na Dk.
Ali Mohamed Shein wa visiwani na pia alimteua kada mkongwe, Abdullahman
Kinana kuwa Katibu Mkuu mpya wa CCM.
Wengine
wanaounda Sekretarieti ni Zakhia Meghji, Mwigulu Nchemba, Asha-rose
Migiro, Vuai Ali Vuai, Nape Nnauye na Mohamed Seif Khatib.
Akimchambua
mmoja baada ya mwingine, Dk. Slaa alimtuhumu Mangula kuwa ni mmoja wa
watu waliohusika na ufisadi wa fedha za Akaunti ya Malipo ya Nje (EPA)
katika Benki Kuu ya Tanzania.
“Makamu
Mwenyekiti Mangula anahusika na EPA, vimemo vingi vya kutaka fedha za
EPA vimetokea kwake…sioni leo atajisafishaje kuleta tumaini jipya kwa
Watanzania,” alisema.
Kuhusu
Meghji, Dk. Slaa alisema huyo ndiye aliyeandika barua na kudanganya kuwa
fedha hizo za EPA zimetoka kwa ajili ya Usalama wa Taifa.
“Sasa mtu kama huyo aliyedanganya, leo hii ukamweka kwenye fedha maana yake ni ku-‘recycle material’ ile ile,” alisema Dk. Slaa.
Akimchambua
Katibu Mkuu, Kinana, alisema kigogo huyo ana mkono katika biashara chafu
za makampuni ya meli na kwamba hajakanusha mpaka sasa.
Dk. Slaa
alisema Kinana ambaye alikuwa meneja kampeni wa mgombea urais wa CCM
mwaka 2010, katika chaguzi hizo CCM imeshutumiwa kwa kuiba kura, hivyo
uteuzi wake ni kukubali kuzika demokrasia nchini.
Alisema timu hiyo imeundwa mahsusi kwa ajili ya kujiandaa kuiba kura mwaka 2015.
Dk. Slaa
aliongeza kuwa baada ya uchaguzi, CCM walitumia fedha nyingi kwa ajili
ya kwenda kufanya utafiti wa kukijenga upya chama chao, ambao uliozaa
kauli mbiu ya ‘Kujivua Gamba’, kwamba pamoja na kazi ya kitaalamu
wameshindwa kuvuana magamba.
Alifafanua kuwa hatua hiyo inatokana na ukweli kwamba walioitwa magamba sasa wamo kwenye safu mpya ya uongozi wa CCM.
Katika kile
kinachoonekana kuwa ni kumjibu Rais Kikwete hasa kutokana na kauli yake
kuwa wapinzani wanafanya kazi ya kueneza uongo na kuwataka makada wa CCM
kujibu mapigo, Dk. Slaa alimtaka aache kuwadanganya Watanzania.
Dk. Slaa alisema kuwa Rais Kikwete huenda hasomi, anadanganywa au anapenda lugha rahisi za kusema wenzake waongo.
“Mawaziri
wameutumia Mkutano Mkuu kwa mbwembwe kueleza uongo…katika ripoti ya Juni
2012, hali ya uchumi wa taifa, iliyoandikwa na Ofisi ya Rais, Ofisi ya
Mipango, na kelele zote zilizopigwa kuhusu maendeleo yaliyopatikana
kwenye barabara.
“Kwenye
ripoti hiyo imeandikwa kuwa mwaka 2011 barabara zilizokuwa katika hali
nzuri ni kilomita 5,976 sawa na asilimia 30.4 ya barabara zote za
mikoa,” alisema.
Ukilinganisha
na mwaka 2010, barabara zilizokuwa na hali nzuri ni kilomita 11,012,
maana yake ni kuwa nusu ya barabara zilizokuwa nzuri mwaka 2010 leo
mwaka mmoja baadaye ni mbaya.
Aliongeza kuwa wakizitumia takwimu hizo ambazo zimeandikwa na Ofisi ya Rais, bado wanaambiwa ni waongo.
Alisema
itakumbukwa kwenye viwanja vya Mwembe Yanga wakati alipotoa orodha ya
mafisadi, Rais Kikwete alimjibu kuwa kelele za mlango hazimzuii mwenye
nyumba kulala lakini leo amekiri ufisadi upo CCM.
Mwanasiasa
huyo machachari, alisema kuwa Rais Kikwete amesikika mara kadhaa
akilalamika kuhusu ufisadi ndani ya chama chake na kuhoji kati yake yeye
na Kikwete nani muongo?
“Aidha Rais sio makini; anapenda maneno rahisi…tunamwambia aweke hadharani takwimu asilete propaganda,” alisema.
Slaa
alikumbusha pia jinsi ambavyo Rais Kikwete na CCM walivyowaita ni waongo
wakati CHADEMA walipokuja na sera ya matumaini kwa Watanzania mwaka
2010, wakisema nyumba za tembe na nyasi sasa basi na kueleza mikakati
yao ya kushusha bei ya saruji na vifaa vya ujenzi.
Katika hilo
Dk. Slaa alisema kuwa alifurahi juzi kusikia CCM katika maazimio ya
Mkutano Mkuu wao wakisema kuwa watashusha bei ya saruji na vifaa vya
ujenzi.
“Sasa CCM na
CHADEMA nani waongo? Mimi nasema hakuna kitu kinachotushangaza katika
uongozi wa sasa, timu ni ile ile ya mafisadi,” alisema
Aliwataka Watanzania kuwa makini akidai kuwa waliowekwa kwenye safu ya uongozi CCM ni mafundi wa ufisadi na kutoa wito kuwa wajiandae kulinda kura.
Naye Katibu
Mkuu wa NCCR-Mageuzi Samuel Ruhuza, alisema wao kama chama wanawapongeza
CCM lakini kwa jicho la siasa hawaoni kipya na kwamba viongozi wapya ni
wachovu wale wale.
“Hawana
jambo jipya kwa sababu CCM imechoka sana haina watu wapya ni walewale,
sasa hivi tulitegemea vijana wapya lakini hilo halijatokea,” alisema
Ruhuza.
JK awasuta wabaya CCM
Mwenyekiti
wa Chama cha Mapinduzi Taifa (CCM), Rais Jakaya Kikwete, amewashambulia
wanachama wa chama hicho waliokuwa na ndoto za kuona mkutano mkuu wao
ukimalizika kwa mpasuko, akisema kuwa wameshindwa.
Rais Kikwete
alitoa kauli hiyo jana ikiwa ni siku moja baada ya kuiteua sekretarieti
ya chama hicho, itakayoongozwa na Katibu Mkuu, Abdullahman Kinana.
Akiwatambulisha
rasmi wateule hao, Rais Kikwete alisema anawashangaa baadhi ya
wanachama ambao wanaifahamu vizuri CCM lakini walikuwa wakiombea mabaya
ili mkutano umalizike vibaya waweze kujivunia kile walichokikusudia.
“Namshukuru
sana Mungu tumemaliza salama; kuna watu walikuwa wakitambika usiku na
mchana CCM imalize vibaya mkutano wake na walitamani itoke na vipande
lakini wameshindwa na sijui watamdai nani gharama zao?” alihoji.
Alisema watu
hao wamepoteza muda wao bure na CCM imara imeweza kumaliza mkutano wake
vizuri na kupanga safu ya ushindi katika uchaguzi wa serikali za mitaa
pamoja na kuingia Ikulu mwaka 2015.
“Nimesikia
mambo mengi na kuna watu kabisa walikuwa wakinijia wakiniambia kuwa kuna
jambo hili na hilo, lakini nilikuwa nawaambia kuwa watulie kwani kuna
watu wana ndoto za mchana wanatumia nguvu nyingi, wanatumia muda wao
bure na wanapoteza wakati wao,” alisema.
Rais Kikwete
alitamba kuyatekeleza maazimio yote waliyoazimia moja baada ya lingine
ili kuhakikisha wanayatimiza kwa wakati na kwa muda mfupi ili Watanzania
kuendelea kujenga imani na chama hicho.
Alisema
wajumbe wa NEC wanatakiwa kutumia muda wao mwingi kuifanya kazi ya chama
ili kuweza kukijenga chama hicho kwa kiwango kikubwa.
Chanzo: Tanzania Daima