Maximo atua Dar na dege la Waarabu





Na Saleh Ally
KOCHA Marcio Maximo anatarajiwa kutua nchini kesho Jumanne majira ya saa 9 Alasiri kufanya mazungumzo ya mwisho kwa ajili ya kuanza kuinoa Yanga.
Maximo, raia wa Brazil, kocha wa zamani wa Taifa Stars, anatarajiwa kutua nchini akiwa kwenye dege la Emirates linalomilikiwa na Falme za Kiarabu, ambalo pia linaidhamini Klabu ya Arsenal ya England.

Habari za uhakika kutoka ndani ya Yanga zimeeleza kuwa tayari klabu hiyo imetuma tiketi ya ndege kwa kocha huyo kutoka Brazil kupitia Dubai hadi Dar na amethibitisha kuipokea.
“Tayari Maximo ana tiketi mkononi na amethibitisha anakuja. Ila kuna kitu kimoja ametuambia kuwa iwapo atashindwa kutua hapa Jumanne, basi siku inayofuata, Jumatano atawasili Dar,” kilieleza chanzo.
“Sijawa na uhakika kama atakuja na msaidizi wake, lakini awali alieleza angependa kuwa na msaidizi mmoja kutoka Brazil kama ilivyokuwa kwa yule Itamar (Amorim).”
Habari nyingine zinaeleza kuwa mara baada ya kutua, Maximo atafanya mazungumzo na Yusuf Manji kesho hiyohiyo au keshokutwa na kama mambo yataenda poa, atasaini mkataba wa kuinoa Yanga.
Yanga ilianza kufanya mazungumzo na Maximo wiki mbili zilizopita, walipokubaliana akawataka wazungumze na timu yake ya Democrata kama itakubali kumuachia. Championi ndiyo lilikuwa la kwanza kuandika kuhusiana na ujio wa kocha huyo.
Mazungumzo na klabu yake yamefanyika kwa takribani siku tatu na juzi uongozi wa Democrata ulimruhusu Maximo kufanya mazungumzo na Yanga kuhusiana na maslahi na kama wakikubaliana atue Jangwani, wao hawana kipingamizi.
Habari nyingine za uhakika zinasema tayari Manji amefanya mazungumzo na Maximo na kumhakikishia kuhusiana na suala la mshahara na makazi ya uhakika Masaki, Oysterbay, Msasani au Mikocheni jijini Dar.
Manji amemwambia Maximo aondoe hofu kuhusu suala la mshahara na amemtaka kuanza kazi ya kuinoa Yanga mara moja kwa ajili ya michuano ya Kagame.
Katika hatua nyingine, Katibu wa Baraza la Wazee, Ibrahim Akilimali, jana mchana aliitisha kikao cha baraza hilo kikiwa na ajenda kadhaa, mbili muhimu ni kujadili ushiriki wa timu hiyo katika Kombe la Kagame, pia mapokezi ya Maximo yatakavyokuwa kesho au Jumatano.