MGOMO WA MADAKTARI WAANZA RASMI

Mgonjwa akihamishwa kutoka Wodi ya Kibasila katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), iliyopo Dar es Salaam jana, ili kupelekwa katika hospitali nyinyine kutokana na tihsio la kuwepo kwa mgomo wa madaktari
katika hospitali hiyo na nyingine za serikali sehemu mbali mbali nchini wanaodai stahiki zao mbali mbali, kwa madai ya serikali kushindwa kuzitekeleza

MADAKTARI nchini wameanza mgomo katika baadhi ya hospitali nchini baada ya Serikali kushindwa kutekeleza madai yao waliyowasilisha katika Kamati ya Majadiliano iliyoundwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.  Mgomo huo umetangazwa na Jumuiya ya Madaktari nchini huku ikifafanua kwamba kati ya madai kumi waliyotaka yatekelezwe na Serikali, hakuna hata moja lililofanyiwa kazi. 
 Hata hivyo,  jana madaktari hao ambao walikaa vikao vya majadiliano na Serikali kwa siku 90 baada ya kusitisha mgomo wao wa pili, wamesema katika madai yao kumi, hakuna hata moja lililotekelezwa na Serikali.  Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Dk Stephen Ulimboka jana aliwaeleza waandishi wa habari kwamba ili warejee kazini, Serikali inatakiwa kutekeleza madai yao yote na kusisitiza kwamba dai lao la kwanza ni kuitaka Serikali kuboresha huduma za msingi kwa wagonjwa. 
 
“Mgomo umeanza leo na hauna kikomo, lengo ni kuishinikiza Serikali kutekeleza madai yetu, hata zile huduma za dharura nazo kuanzia kesho (leo) zinaweza kusitishwa,” alisema Dk Ulimboka.  Wakati Ulimboka akieleza hayo, huduma katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) na Taasisi ya Mifupa (Moi) ilikuwa ikitolewa kwa kusuasua huku baadhi ya wafanyakazi wakisisitiza kuwa mgomo huo upo.