MAREKANI imeungana na Uingereza kushinikiza kutambuliwa kwa haki za mashoga, ikitumia rungu la misaada yake inayotoa kwa nchi mbalimbali duniani, huku ikitenga Dola za Marekani 3 milioni sawa na Sh5.1bilioni, kwa ajili ya kufanikisha mkakati huo.
Shinikizo hilo la Marekani ambalo ni taifa kubwa kiuchumi duniani, linazidi kuchochea mjadala ulioibuliwa na Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, ambaye alitangaza katika mkutano wa Jumuiya ya Madola uliofanyika Uswis hivi karibuni kwamba, nchi yake itasitisha misaada kwa nchi zote duniani ambazo hazitambui haki za mashoga.
Baada ya Cameron, Rais Barack Obama wa Marekani naye juzi alitangaza kwamba, taifa hilo kubwa litatumia uwezo wake wote ikiwamo misaada inayotoa kwa nchi mbalimbali kuhakikisha haki za mashoga zinatambuliwa na kuthaminiwa duniani.
Rais Obama alitoa msimamo huo jijini Washington katika hafla ambayo pia ilihudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Nchi hiyo , Hillary Clinton ambaye ndiye alikuwa mzungumzaji mkuu.
“Wengine wanasema kuwa haki za mashoga na haki za binaadamu ni vitu tofauti na havifanani, lakini ukweli ni kwamba ni kitu kimoja na chenye usawa,”alisema Clinton wakati akisoma taarifa hiyo maalumu yenye baraka za Obama.
Clinton alisema, “Tayari tumetenga kiasi cha Dola za Marekani 3 Milioni kwa ajili ya programu ya kutangaza haki za mashoga ili kuondokana na ubaguzi na unyanyasaji dhidi yao.”