AJALI
ya kuzama kwa Boti mali ya kampuni ya Seagull July 18, 2012 ilizua hali
ya kwanini ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, baada ya
Spika wa Bunge, Anne Makinda kukataa hoja ya kutaka kujadili suala la
ajali hadi pale taarifa kamili zitakapotolewa hivyo mjadala wa Bajeti ya
Wizara ya mambo ya Ndani uendelee.
Kutokana
na ajali hiyo, muda mfupi baada ya kipindi cha jioni kuanza, Mbunge wa
Wawi (CUF), Hamad Rashid Mohamed alisimama na kuomba mwongozo kwa
kutumia Kanuni ya 47(3) kulitaka Bunge lipitishe Makadirio ya Matumizi
ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mafungu bila ya kutolewa
ufafanuzi ili wabunge waweze kupata muda wa kujadili tukio hilo.
Hata
hivyo, Spika Anne Makinda alipinga hoja ya Hamad na kutaka Bunge
liendelee akieleza kwamba kanuni hiyo imekuwa ikitumiwa vibaya na kwamba
tayari ameshawasiliana na waziri husika na kwamba taarifa kamili
zitakapopatikana angelitaarifu Bunge.
Baada ya kauli hiyo Spika Makinda aliruhusu shughuli za Bunge ziendelee na kumwita Silima kutoa ufafanuzi wa hoja za wabunge.
Lakini wakati Naibu Waziri huyo akielekea kutoa hotuba yake, wabunge wote wa CUF, Chadema na baadhi wa CCM walitoka nje na kwenda katika Ukumbi wa Msekwa ili kupeana taarifa za ajali hiyo na kupanga mikakati ya jinsi ya kutuma ujumbe wa haraka kwenda Zanzibar kushirikiana na waokoaji.
Ukumbi huo uligeuka kuwa wa maombolezo kwa muda baada ya wabunge wengi kuangua vilio pale walipopewa taarifa rasmi za ajali hiyo.
Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid alieleza kwa ufupi tukio lilivyo na kwamba wangemwomba Waziri Mkuu, Mizengo Pinda awasaidie ndege ya Serikali ili waweze kwenda Zanzibar kujumuika na wenzao katika tukio hilo.
Baada ya Hamad kumaliza alisimama Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia ambaye alijaribu kuwatuliza wabunge akisema kuwa, meli inaweza kuzama lakini watu wasipoteze maisha kutokana na kuchukua muda, kauli ambayo ilipingwa na wabunge wengi.
Mbunge wa Mji Mkongwe (CUF), Ibrahim Sanya alimshutumu Spika Makinda akisema, amekosa hisia na hajui kwamba kuzama kwa meli ni janga la kitaifa.
“Kwa hili hata nikikutana na Spika nitamwambia kweli ameniudhi. Sihitaji ubunge kama hali yenyewe ndiyo hii na tutapiga kura ya kutokuwa na imani na Spika,” alisema Sanya.
Wakati hayo yakitokea, katika Viwanja vya Bunge baadhi ya wabunge na mawaziri walionekana wakiwa katika vikundi wakijadili suala hilo, huku wengine wakipinga uamuzi huo wa Spika.
Wakati hayo yakiendelea katika Ukumbi wa Msekwa, Bunge lilikuwa likiendelea kumsikiliza Silima akijibu hoja za wabunge na baada ya kumaliza, Spika Makinda alimwita mtoa hoja, Waziri Nchimbi naye kujibu.
Lakini badala yake, alitumia fursa yake kuondoa hoja ya Makadirio ya Matumizi ya wizara yake ili kutoa fursa kwa Bunge kujadili ushiriki wake katika tukio la kuzama kwa boti hiyo.
Dk Nchimbi alitumia Kanuni ya 58 (5) ambayo inamtaka mtoa hoja kusimama na kutoa hoja ya kuondoa mezani hoja yake kama kuna jambo la dharura.
“Mheshimiwa Spika, natumia Kanuni ya 58 (5) ambayo inamtaka Waziri kusimama na kutoa hoja ya kuondoa mezani hoja yake kama kuna jambo la dharura,” alisema Dk Nchimbi.
Dk Nchimbi aliendelea: “Ikumbukwe Mheshimiwa Spika, muda mfupi kabla ya kuingia hapa ndani uliniita mimi na Naibu Waziri ukataka tukueleze hali ya ajali hiyo na kwa wakati huo Kamishna wa Matukio Zanzibar alikuwa eneo la tukio. Sasa basi, kutokana na agizo lako, ni imani yangu kwa muda aliotumia Naibu Waziri unatosha kuendelea kufuatilia jambo hilo.”
Baada ya kutoa maelezo hayo, Wabunge wote 49 waliokuwa wamebaki katika ukumbi walisimama kuunga mkono hoja.
Baada ya hapo, Spika Makinda aliwahoji na kwa kauli moja waliridhia kuahirishwa kwa kikao hicho wakati huo ikiwa saa 11:31 hadi leo saa 3.00 asubuhi, huku akiitisha kikao cha dharura cha Kamati ya Uongozi ya Bunge jana hiyohiyo kujadili suala hilo.
Akizungumza baada ya kikao hicho cha Kamati ya Uongozi, Kaimu Katibu wa Bunge, John Joel alisema, limeamua kufuta kipindi cha Maswali kwa Waziri Mkuu na kwamba kikao cha Bunge kitaendelea leo asubuhi kuanzia saa 2:00 kupokea taarifa ya Serikali kisha watajadili mustakabali wa vikao vya Bunge.Kamati hiyo pia iliamua kutuma ujumbe wa wabunge kwenda Zanzibar kuwafarijiwa wale wote walioathiriwa na ajali hiyo.
Imeandikwa na Salma Said, Zanzibar, Neville Meena, Habel Chidawali na Boniface Meena, Dodoma; Raymond Kaminyoge, Aidan Mhando, Dar es Salaam. SOURCE: Mwananchi.co.tz