NGORONGORO HEROES YATUA SALAMA NIGERIA.
|
Picha kutoka maktaba. |
Ngorongoro Heroes, timu
ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 imewasili asubuhi hii
(Agosti 10 mwaka huu) kwa ndege ya Overland Airways kwenye mji wa
Ilorin, Jimbo la Kwara lililo Kusini mwa Nigeria tayari kwa mechi ya
marudiano dhidi ya wenyeji Flying Eagles itakayochezwa Jumapili. Mechi
hiyo ya raundi ya pili ya michuano ya U20 ya Afrika itachezwa kwenye
Uwanja wa Township kuanzia saa 10 kamili jioni kwa saa hapa ambapo
Tanzania itakuwa ni saa 12 kamili jioni. Ngorongoro Heroes ilitua jana
(Agosti 9 mwaka huu) jijini Lagos ambapo ililala kabla ya kuja
hapa. Msafara wa Ngorongoro Heroes wenye watu 27 ukiongozwa na mjumbe wa
Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mtwara
(MTWAREFA) ulipokea na Ofisa Ubalozi wa Tanzania nchini Nigeria, Jones
Mndeme na viongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Nigeria (NFF)
umefikia hoteli ya Kingstone Grand Suites. Kwa mujibu wa Kocha wa
Ngorongoro Heroes, Jakob Michelsen, timu itafanya mazoezi leo jioni
(Agosti 10 mwaka huu) wakati mazoezi ya mwisho yatakuwa kesho jioni
(Agosti 11 mwaka huu) kwenye uwanja ambao utatumika kwa mechi ya
Jumapili. Wachezaji wote wako katika hali nzuri isipokuwa Issa Rashid na
Aishi Manula ambao walikuwa wakisumbuliwa na tumbo baada ya timu kufika
jana (Agosti 9 mwaka huu) jijini Nairobi, Kenya ambapo ilibadili ndege
kuja Nigeria. Hata hivyo, hali zao zinaendelea vizuri na huenda wakawa
sehemu ya kikosi cha kwanza kitakachoivaa Flying Eagles. Mbali ya Rashid
na Manula, wachezaji wengine walioko hapa kwenye kikosi cha Ngorongoro
Heroes ni Barwany Khomeiny, Samir Ruhava, Dizana Yarouk, Leonard
Muyinga, Hassan Ramadhan, Jamal Mroki, Omari Kheri, Frank Domayo,
nahodha Omega Seme, Abdallah Kilala, Hassan Dilunga, Ramadhan Singano,
Simon Msuva, Said Zege, Atupele Gren na Ramadhan Salum. Mbali ya
Michelsen, Benchi la Ufundi linaundwa na Mohamed Rishad 'Adolf' (Kocha
Msaidizi), Peter Manyika (Kocha wa makipa), Nassoro Matuzya (Daktari),
Joakim Mshanga (Physio), Juma Kizwezwe (Mtunza vifaa) na Meneja wa timu
John Lyimo. Flying Eagles ambayo ilishinda mechi ya kwanza mabao 2-1
nayo tayari imeshaingia hapa Ilorin ikitokea Lagos kwa mechi hiyo ambayo
matokeo yake yataamua timu ipi itaingia raundi ya tatu ambayo ni ya
mwisho kabla ya fainali za Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka
20 zitakazofanyika mwakani nchini Algeria. Timu itakayovuka itacheza
raundi hiyo na mshindi kati ya Congo Brazzavile na Afrika Kusini.