Bodi
ya Wadhamini ya Hospitali ya Taifa Muhimbili ilikutana tarehe 28 Juni
2012 kujadili na kutathmini hali ya utendaji na utoaji wa huduma hivi
sasa katika Hospitali. Imebainika kwamba utoaji huduma umeathirika
kutokana na mgomo wa baadhi ya madaktari unaondelea kwa takriban wiki
moja sasa tangu ulipoanza Jumamosi yatarehe 23 Juni 2012.
Baada ya tathmini hiyo, Bodi ya Wadhamini imeagiza yafuatayo:
(i) Madaktari waliopo kazini waendelee na kazi kama kawaida;
(ii)
Madaktari waliogoma warejee kazini kutii amri ya Mahakama Kuu Kitengo
cha kazi, kwa mujibu wa Kifungu Na. 76 (1) na (2) cha Sheria ya Ajira na
Mahusiano Kazini ya mwaka 2004.
(iii) Madaktari waliopo likizo warejee kazini mara moja. Utaratibu wa kufidia likizo na nauli zao umeandaliwa.
(iv)
Uongozi wa Hospitali uwachukulie hatua za kinidhamu wafanyakazi wote
watakaoendelea kutokuhudhuria kazini na kufanya kazi bila sababu za
msingi kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na taratibu za kazi;
(v) Uongozi wa Hospitali ufute mara moja ‘rotations’ za Madaktari waliopo kwenye mafunzo kwa vitendo (interns); na
(vi)
Uongozi wa Hospitali uwapange (re-deploy) Madaktari na Madaktari Bingwa
waliopo kwenye maeneo yaliyoathirika wakati huu wa mgomo.
Aidha,
Bodi ya Wadhamini inawashukuru sana madaktari na wafanyakazi wote ambao
wameendelea kuwahudumia wagonjwa wetu na wananchi kwa ujumla. Vilevile,
Bodi ya Wadhamini inawasihi madaktari na wafanyakazi wote wawe na
subira na waheshimu sheria, kanuni na taratibu zilizopo pamoja na
maadili ya taaluma zao.
_________________
Dkt. Gabriel Upunda
KAIMU MWENYEKITI
BODI YA WADHAMINI