Iringa
imezinduka kwenye michuano ya Copa Coca-Cola baada ya leo asubuhi (Juni
30 mwaka huu) kuifunga Kaskazini Pemba mabao 3-0 katika mchezo
uliofanyika Uwanja wa Nyumbu mkoani Pwani.
Hadi
dakika 45 za kwanza za mechi hiyo ya kundi B zinamalizika matokeo
yalikuwa suluhu. Mabao ya washindi yalifungwa na Goodluck Jonas dakika
ya 51, Musa Maginga dakika ya 67 na Ramadhan Kiwelu dakika ya 70.
Iringa
ilipoteza mechi zote mbili za kwanza dhidi ya Mwanza na Mjini
Magharibi. Mbele ya Mwanza ilifungwa 3-1 wakati kwa Mjini Magharibi
ikachezea kichapo cha mabao 3-0.
Katika
mechi nyingine zilizochezwa asubuhi, Tabora iliichapa Shinyanga mabao
2-0 kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam. Mabao hayo
yalifungwa na Said Juma na Ramadhan Mbalamwezi katika kila kipindi.
Nayo
Ilala imepata pointi yake ya kwanza katika michuano hiyo baada ya
kutoka suluhu na Kusini Pemba katika mechi ya kundi A iliyochezwa Uwanja
wa Tanganyika Packers ulioko Kawe, Dar es Salaam. Mjini Kibaha mkoani
Pwani kwenye Uwanja wa Tamco, Dodoma iliibuka na ushindi wa bao 1-0
dhidi ya Mtwara.