MNADHIMU
wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu ameingia matatani kutokana na
kauli yake kwamba Rais Jakaya Kikwete amekuwa akiteua majaji wa
Mahakama Kuu wasiopendekezwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama.
Kutokana
na kauli hiyo aliyoitoa wakati akiwasilisha maoni ya kambi yake, kuhusu
hotuba ya makadirio ya matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria, Lissu
ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema) atajadiliwa na
Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge.
Wakati
akisoma hotuba yake, mbunge hiyo alisema majaji wanaoteuliwa na Rais
hawafanyiwi ‘vetting’ (uchunguzi) na tume hiyo kuona kama uwezo na ujuzi
wao unafaa kukabidhiwa madaraka ya ujaji.Mwenyekiti wa Bunge, Jenista
Mhagama ndiye aliyeamuru suala la Lissu kupelekwa katika kamati hiyo
baada ya mbunge huyo kukataa kufuta kauli yake ambayo kwa mtazamo wa
Serikali iliwadhalilisha majaji.Hata hivyo, jana alipotakiwa kueleza
kama ana taarifa rasmi za kuitwa kwenye kamati hiyo Lissu alisema:
“Sijaitwa,
lakini nina taarifa kuwa naweza kuitwa.’’Alisema, hata wakimwita
hatakuwa na jambo lolote la kuzungumza kwa kuwa Mwenyekiti wa Bunge
aliyeongoza kikao hicho juzi (Jenista Mhagama), alikosea kwa kuwa ndiye
aliyepaswa kumpa adhabu.Mbunge huyo alisema juzi aligoma kufuta kauli
yake kama alivyotakiwa na Mwenyekiti kwani aliamini kuwa hata
Mwanasheria Mkuu alikuwa amekosea.Alibainisha kuwa endapo ataitwa katika
kamati hiyo, atahoji kama waliomwita wamegeuka kuwa wenyeviti wa Bunge
na kama si hivyo, anaamini watakosa neno la kumhoji.Waziri wa Katiba na
Sheria, Mathias Chikawe na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick
Werema kwa nyakati tofauti wakati wakijibu hoja za wabunge juzi jioni
walisema: “Lissu aliwakashifu majaji bungeni, hivyo alipaswa kuomba
radhi.”Kwa upande wake Werema alimtaka Lissu kufuta kauli yake na kwamba
ikiwa hatafanya hivyo basi awasilishe vielelezo vinavyothibitisha madai
kwamba majaji huteuliwa bila kufanyiwa uchunguzi.“Lissu ni mtaalamu wa
sheria, lakini kauli yake imewafedhehesha majaji na inashangaza
inapotolewa na wakili machachari kama yeye,” alisema Werema.Werema pia
alimtaka Lissu kuondoa kauli yake kwa kuwataja watu ambao sio wabunge
kwa kunukuu gazeti la Mwanahalisi lililowataja watu watatu kuwa
wamehusika na mauaji ya Dk Steven Ulimboka.Werema alisema iwapo Lissu
hataondoa maneno yake suala hilo lipelekwe katika Kamati ya Maadili.Kwa
upande wake, Chikawe alimwombea radhi Lissu kwa majaji akisema anajua
hakutoa kauli ya kuwadhalilisha majaji kwa kukusudia.“Lissu amemtuhumu
hadi Rais katika uteuzi wa majaji, hili siyo sahihi, uteuzi wa majaji
hupendekezwa na tume maalumu inayohusisha majaji wazoefu ambao ndio
wanapendekeza majina kwa Rais,” alisema Chikawe.Baada ya maelezo hayo,
Mhagama aliamuru Lissu kuondoa kauli yake hiyo baada ya kutakiwa kufanya
hivyo na Werema wakati akifanya majumuisho ya mjadala wa wizara
hiyo.Hata hivyo, Lissu alipopewa nafasi alisema hawezi kuondoa kauli
yake kwa kuwa mchakato mzima wa kumtaka afanye hivyo haukufuata Kanuni
za Bunge.Lissu alinukuu kanuni ya 63 (1) ambayo inasema: “Bila kuathiri
masharti ya Ibara ya 100 ya Katiba yanayolinda na kuhifadhi uhuru wa
mawazo na majadiliano katika Bunge, ni marufuku kabisa kusema uongo
bungeni kwa sababu hiyo, mbunge yeyote anapokuwa akisema bungeni ana
wajibu wa kuhakikisha kwamba anatoa kauli au maelezo kuhusu jambo au
suala ambalo yeye mwenyewe anaamini kuwa ni kweli na siyo jambo la
kubuni au la kubabaisha tu”.Lissu aliongeza kuwa, Jaji Werema na Mhagama
walivunja Kanuni za Bunge kwa kumtaka kuondoa kauli inayodaiwa kuwa ya
uongo kinyume bila kufuata utaratibu.Alipoulizwa kuhusu utekelezaji wa
hatua hiyo jana, Mkuu wa Serikali Jaji Fredrick Werema alisema kuwa siyo
lazima kwa Watanzania kufahamu hilo.“Nilipozungumza jana (juzi)
sikuzungumza na Watanzania bali nilizungumza na Bunge, hivyo siyo lazima
Watanzania kufahamu jambo hilo na wala sioni sababu za kwa nini
liandikwe magazetini,’’ alisema Jaji Werema.
Source from Mwananchi.co.tz
Source from Mwananchi.co.tz