Maisha Plus kurejea mwezi ujao


Ile reality show iliyokuwa imejipatia umaarufu nchini ya Maisha Plus inatarajiwa kurudi kwenye runinga kwaajili ya msimu wa tatu.
Taarifa ambayo hata hivyo sio rasmi imetolewa jana na mwanzilishi wa Maisha Plus, Masoud Kipanya kupitia mtandao wa Twitter.
Kipanya alitoa taarifa hiyo baada ya kuulizwa swali na mtu aliyetaka kujua kama kuna mipango yoyote ya kuirejesha show hiyo.
Mchoraji huyo maarufu wa katuni ya Kipanya ya gazeti la Mwananchi alisema kuwa maandalizi yameshaanza.

“Tunaanzia Arusha early August. Matangazo yataanza soon on TBC and local (Arusha) radios,” alisema Masoud.
Aliongeza kuwa baada ya usaili wa kusaka washiriki kwenye mikoa mbalimbali nchini, kijiji kinatarajiwa kuanza mwezi Oktoba.
Ni mwaka wa pili sasa tangu Maisha Plus iruke kwa mara ya mwisho na ambapo ilimalizika ikiwa na kasoro kadhaa.
Miongoni mwa kasoro ambazo watazamaji walikuwa wakizisema ni pamoja na show hiyo kukosa uhalisia kama inavyotakiwa kuwa, huku washiriki wengi wakionekana kuigiza badala ya kuishi maisha ya kawaida.