Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi akitoa ufafanuzi wa
ajali ya Meli ya M.V.Skagit kwa Wabunge wa Muungano waliofika Zanzibar
kuwafariji wafiwa na majeruhi waliopata ajali hiyo. Kushoto kwa Balozi
ni Spika wa Bunge la Muungano Anna Makinda na Mbunge wa Mafia, Abdull
Razak. Kulia ya Balozi ni Mbunge wa Jimbo la Magomeni Mjini Zanzibar,
Mohd Amour Chombo
Wabunge
wa Muungano wakifuatilia maelezo ya makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Balozi Seif Ali Iddi kuhusu ajali ya meli ya M.V Skagit katika ukumbi
wa juu wa Baraza la Wawakilishi Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Serikali
zote mbili ya Muungano na ile ya Mapinduzi ya Zanzibar zimeziagiza
Mamlaka zinazosimamia usafiri wa Baharini za Sumatra ya Tanzania Bara
na ZMA ya Zanzibar kufanya kazi kwa mashirikiano zaidi ili kupata
ufanisi na kuondoa kasoro zinazoweza kuleta hitilafu ya kiutendaji.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo
wakati akizungumza na Timu ya Wabunge wa Bunge la Muungano hapo ukumbi
wa juu wa Baraza la Wawakilishi Mbweni ambao
walifika Zanzibar kutoa mkono wa pole kufuatia ajali ya Meli ya M.V Skagit iliyotokea kati kati ya wiki hii.
Balozi Seif aliueleza Ujumbe wa Wabunge hao walioongozwa na Spika wake
Mh. Anna Makinda kwamba mashirikiano hayo yanaweza kusaidia kwa kiasi
kikubwa kuwepuka hitilafu za vyombo wakati vinapotoa huduma ya usafiri
kwa abiria wa pande zote mbili.
“ Baadhi ya Wafanyabiashara wetu wamekuwa na tabia ya kutuletea vyombo
kachara vilivyochakaa kutoa huduma ipasavyo ambavyo ni hatari kabisa
kuvitumia kwa maisha ya wasafiri wetu”. Alieleza Balozi Seif Ali Iddi.
Alisema Serikali hizo zimesisitiza kwamba kazi za mashirikiano hayo kwa
mamlaka hizo ni vyema zilenge zaidi katika shughuli za upasishaji wa
vyombo husika.
“ Itapendeza na kujenga mazingira bora inapotokezea mamlaka moja ikitoa
maamuzi kuhusiana na chombo chenye hitilafu ya kiufundi na ile ya Pili
kuweka baraka zake. Hii inatokana na sababu ya vyombo hivyo vya
usafiri kuhudumia Wananchi wa pande zote mbili”.Alisisitiza Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar.
Balozi Seif alieleza kwamba Serikali itajitahidi kwa kufanya uchunguzi
wa kina na kitaalamu kuona iwapo vyombo vya usafiri vilivyopo hivi sasa
vinafaa kuendelea kutoa huduma.
Akizungumzia suala la janga la Meli ya M.V Skagit Balozi Seif aliueleza
Ujumbe wa Wabunge hao wa Bunge la Muungano kwamba Wazamiaji wa Israel
walioko katika Hoteli ya Kitalii Nungwi kwa kushirikiana na Timu ya
wazamiaji wazalendo wanaendelea na zoezi la kuitafuta Meli hiyo ya M.V
Skagit.
Alisema zoezi hilo la uchunguzi wa kuitafuta Meli hiyo lilianza jana
katika eneo ilipozamia la karibu na Kisiwa cha Chumbe bila ya mafanikio
licha ya kina kidogo cha maji cha Mita 30 hadi 38 ikilinganisha na kile
cha Mkondo wa Nungwi.
Alisema siku tatu za maombolezo
zimemalizika hivyo amewakumbusha waumini wa Dini na madhehebu mbali
mbali pamoja na Wananchi kuwaombea dua katika majengo yao ya Ibada hapo
kesho wale
marehemu waliotangulia mbele ya haki kutokana na ajali hiyo.
Balozi Seif
alifafanua kwamba Serikali imeshatoa ruhusa kwa Wananchi watapozipata
maiti za wahanga wa ajali hiyo kuizika sehemu hiyo hiyo kulingana na
muda ulivyopita.
Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar aliupongeza Ujumbe huo wa Wabunge ukiongozwa na Spika
Makinda kwa kitendo chao cha kuja kufariji wafiwa ambacho
kinathibitisha kuguswa kwao na tukio hilo.
Akitoa shukrani kwa
Niaba ya Timu ya ujumbe wa Wabunge hao Mbunge wa Jimbo la Magomeni Mh.
Mohd Amour Chombo amezipongeza jitihada za Serikali zote mbili
zilizochukuliwa katika kukabiliana na janga hilo.
Mh. Chombo alisema hatua hiyo ya muda mfupi imesaidia kunusuru vifo na majeruhi kadhaa wa ajali ya Meli hiyo ya M.V Skagit.
Hadi jana jioni
wazamiaji kwa kushirikiana na Vikosi vya Ulinzi vya pande zote mbili
Nchini wameweza kuokoa jumla ya Maiti 68 na waliohai ambao wengine
walipata majaraha 146.
Na
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar