Mama Amuuza Binti Yake Ili Anywe Bia


WESTERN CAPE, Afrika Kusini


POLISI katika mji wa Western Cape nchini Afrika kusini bado wanamuwinda mwanamke anayedaiwa kumgeuza bintiye mwenye umri wa miaka 13, kuwa mtumwa wa mapenzi kwa kumuuza kwa Randi 50 (shilingi 6000) na kutumia fedha anazozipata kunywea pombe.

Mwanamke huyom anadaiwa kuwa mara kwa mara alikuwa akimchukua msichana huyo na kumpeleka vichakani  au nje ya mji na kumuuza kwa wanaume mbalimbali. H ata hivyo anadaiwa kuwa alikuwa mlevi na mtumiaji wa madawa ya kulevya na kusababisha mtoto huyo kubakwa mara kwa mara.
Madai ya unyanyasaji kuhusu mtoto huyo yalijulikana  baada ya mtoto huyo kumwambia mmoja wa marafiki zake, ambaye aliamua kumweleza suala hilo mwalimu wao. Mtoto huyo kwa sasa amehifadhiwa katika makazi ya wakimbizi ya Atlantis akipatiwa ushauri nasaha na mshauri Barbara Rass.
"Ninampongeza mwalimu, kwani amevunjwa ukimya uliokuwa umegubikwa. Ni kama kila mmoja sasa anajua nini kilichokuwa kikiendelea, hakuna mtu ambaye angetambua kama kuna lolote linaendelea kama yeye asingemweleza rafiki na kisha mwalimu kujua jambo hilo," alisema Rass.
Siku ya Jumatatu, kesi ilifunguliwa rasmi na polisi ambao waliendelea kuchunguza madai hayo ya kesi ya ubakaji na kumwingiza mtoto katika biashara ya ukahaba.
Rass mwenye umri wa miaka 35 ana uzoefu katika kesi mbalimbali zinazofunguliwa na jamii na waathirika wa mashambulizi na vitendo vya ngono, alikuwa akilia wakati akielezea kuhusu kesi hiyo ya kutisha.
Alisema binti huyo alimweleza jinsi mama yake alimpeleka katika madanguro mbalimbali ili afanye ngono na wanaume wazee. Vitendo hivyo Rass anasema vilifanywa karibu kila siku usiku wakati binti huyo aliporejea nyumbani akitokea shuleni.
"Mama yake alimchukua na kumpeleka katika madanguro na kumwambia 'huyu ni mwanamume kwa ajili yako'. Au alimpa chokleti na kumwambia 'En hier is vir jou 'n man [na huyu ni mwanamume kwa ajili yako]'. Alikuwa akiondoka na kwenda msituni na mwanamume wakati mama yake akiendelea kunywa pombe," alisema Barbara.
Wakati timu ya Dailyvoice ilipotembelea eneo alilokuwa akiishi mwanamke huyo siku ya Jumanne, Mabinti watano wenye umri sana na binti huyo walikuwa wakitembea sehemu hizo hatarishi pasipo mwongozo wa wazazi. Maeneo hayo ambako malori makubwa hupaki, kulikuwa kumezungukwa na vichaka pamoja na vibanda kadhaa mbavyo inasemekana usiku hugeuzwa madanguro.
Hata hivyo kutokana na ulinzi mkali uliowekwa eneo hilo, mabinti hao waliishia katika mikono ya polisi wiki iliyopita. Lakini  muathirika anasema kuwa yeye alikuwa akiambiwa kuwa asiseme neno lolote kwa mtu mpaka alipofika katika mikono ya Rass na kueleza ukweli wa mambo.
"Licha ya kufika mikono salama bado binti huyo hakutaka kutaja majina ya wanaume waliombaka na kusema kwamba mwanamume wa mwisho kumbaka alikuwa wa kabila la Xhosa. Bado hakutaka kutaja mahali anapoishi wala kuzungumza lolote, kisha akanambia tu baada ya hapo nini kiliendelea" mshauri huyo anaeleza.
Licha ya ukimya uliokuwa umemwandama msichana huyo, hatimaye Jumatano alizungumza namna alivyoteseka katika unyanyasaji aliofanyiwa na mama yake. Alieleza namna alivyofanyiwa ukatili wa kutisha na kuvumilia siku zote.

Chanzo:  http://www.mwananchi.co.tz/habari/Kimataifa