MJADALA WA GOAL-LINE TECHNOLOGY KUHITIMISHWA LEO.

Sepp Blatter.
MJADALA uliochukua karibu miaka kumi kuhusiana na suala la matumizi ya mfumo wa teknologia ya kompyuta katika mstari wa goli katika mchezo wa soka unaweza kufikia tamati leo katika kikao cha Bodi ya Kimataifa ya mchezo wa Soka-IFAB kitakachokaa. Katika kikao cha leo ambacho kitafanyika katika makao makuu ya Shirikisho la soka duniani-FIFA ajenda kubwa itakuwa ni kuzijadili kampuni mbili ambazo mifumo yake imekuwa ikifanyiwa majaribio katika kipindi cha miezi kadhaa. Kutakuwa na kura nane katika kikao hicho cha IFAB ambapo kura nne zitakuwa za wajumbe wa FIFA na kura moja kwa kila nchi wanachama za Uingereza, Scotland, Wales na Ireland ya Kaskazini na kura zinazohitajika kupitisha mfumo mojawapo ni robo tatu ya kura zote. Rais wa FIFA, Sepp Blatter amekuwa akiwahimiza wajumbe wake kukubaliana na mfumo huo kufuatia tukio lililotokea katika michuano ya Ulaya mwaka huu ambapo shuti alilopiga mchezaji wa Ukraine Marco Devi kuonekana limeokolewa na beki wa Uingereza John Terry mpira ukiwa umevuka mstari lakini mwamuzi aliwanyima bao hilo. Mara baada ya tukio hilo Blatter aliandika ujumbe katika mtandao wa kijamii wa twitter kuwa suala la mfumo wa teknologia ya kompyuta katika mstari wa goli ni suala la lazima katika soka la kisasa. Rais wa Shirikisho la Soka la Ulaya-UEFA yeye ameweka imani katika matumizi ya waamuzi watano katika mechi ambapo waamuzi wawili wanakuwa pembeni ya magoli nayo pia inaweza kupitishwa na IFAB leo.