Pinda Atoa Changamoto Kwa Wanafunzi...!

 
Waziri Mkuu Mizengo Pinda akitoa wosia kwa wanafunzi 20 waliofanya vizuri katika mitihani ya kidato cha sita kwa mwaka 2012 bungeni leo mjini Dodoma. Wanafunzi hao 10 wasichana na 10 wavulana wamepewa cheti , kopyuta ya pakato (laptop) na fedha taslimu shilingi laki mbili kwa kila mmoja.Wanafunzi hao 10 wasichana na 10 wavulana wamepewa cheti na Waziri Mkuu, kopyuta ya pakato (laptop) na fedha taslimu shilingi laki mbili kwa kila mmoja.Picha na Anna Nkinda – Maelezo
 Wanafunzi 20 waliofanya vizuri katika mitihani wa kidato cha sita kwa mwaka 2012 wakiwa katika picha ya pamoja nje ya ukumbi wa Bunge leo mjini Dodoma.

WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda amewataka wanafunzi wote nchini kuwa na nidhamu , kujituma na kufuata maelekezo vizuri ya walimu wao na kuepuka makundi mabaya ili kuweza kupata mafanikio katika masomo yao.

Aidha Waziri Mkuu Pinda amewaasa wanafunzi waliofanya vizuri katika mtihani wa kuhitimu kidato cha sita wa mwaka huu kutumia uhuru vizuri watakaoupata kwenye maisha ya vyuo vya elimu ya juu bila kurudi nyuma katika maendeleo ya masomo yao.

Kauli hiyo ilitolewa leo na Waziri Mkuu, Pinda Bungeni mjini Dodoma kabla ya kuwatunuku vyeti vya kuwapongeza wanafunzi hao 19 kati 20 waliofanya vizuri katika mtihani huo,kutoka shule mbalimbali nchini, ambapo mmoja wao, Jamal Juma yuko nje ya nchi.

Wanafunzi hao ambao wote walipata ufaulu wa daraja la kwanza katika mtihani huo, saba kati yao wanatoka katika shule ya wasichana ya Marian, watatu Mzumbe, wawili Fedha na wengine wawili Kibaha. Waliobakia mmoja mmoja anatoka Kilakala, Ufundi Ifunda, Tabora girls, Tabora boys, Minaki na Mpwapwa.

“Mmefanya vizuri. Mnastahili ! Hongereni Sana. Tunataka ufaulu wenu uwe mzuri zaidi kwa vile sasa ninyi mnakweda kujenga weledi. Mnakuwa wataalamu wa fani Fulani. Tumieni muda wenu kujifunza zaidi kutafuta maarifa zaidi na kuvumbua mambo makubwa zaidi yatakayowasaidia ninyi wenywe na jamii kwa ujumla kujiletea maendeleo,” alisema Waziri Mkuu Pinda.

Aliongeza kuwa ni vizuri utaratibu huo wa kuwatambua wanafunzi bora uwe endelevu na ikiwezekana wapatiwe fursa ya kuendelezwa katika vyuo vikuu vya kipekee nje ya nchi hususan kwenye fani zitakazojenga uwezo kwa taifa.

Waziri Mkuu alisema kati ya shule 10 ,ambazo wanafunzi hao wanatoka, wawili ni kutoka shule za kata, ambao ni Ester Marcel toka shule ya sekondari ya wasichana ya Olele Kilimanjaro na Brighton Lema toka shule ya sekondari ya Kitangiri, Mwanza.

“Napenda niwape pongezi za pekee wanafunzi hawa kwa jihudi kubwa walizozionesha. Kufaulu kwao kunadhihirisha kwamba shule hizi za kata tukiweka bidii kwa kuziwezesha zaidi zitafanya vizuri zaidi kama ilivyo katika shule nyingine,” alisisitiza .

Waziri Mkuu pia aliwataka walimu wote nchini kushirikiana na wazazi na serikali kwa pamoja kufundisha watoto kwa bidii ili waweze kufanya vizuri katika masomo yao kama wanafunzi hao waliotunukiwa vyeti hivyo.

Kwa upande wake Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa alisema wanafunzi hao watazawadiwa pakato (laptop) na sh. 200,000, pia kila shule iliyotoa mwanafunzi bora itazawadiwa sh. milioni moja katika hafla maalum itakayofanyika jioni.

Wanafunzi hao wanatoka katika mchepuo wa PCM ambao ni 16 na mmojammoja toka mchepuo wa PGM, CBA, ECA na HKL.

Naye Spika wa Bunge la Jamhuri, Anna Makinda aliwataka wanafunzi hao kuwa makini na makundi kwa kuyasilikiza huku wakitumia akili zao huku akitoa changamoto shule nyingine kujitahidi kufanya vizuri.