FABREGAS ASIFU UWEZO WA WENGER.

KIUNGO wa klabu ya Barcelona, Cesc Fabregas amedai kuwa Arsene Wenger ana kipaji cha kipekee katika kuendeleza wachezaji chipukizi na kusisitiza kuwa mfaransa huyo ataiongoza Arsenal kushinda taji msimu huu. Fabregas ambaye aliondoka Arsenal Agosti mwaka jana anaamini kuwa Wenger mwenye umri wa miaka 62 ana uwezo wa kuwapa ujasiri na kujiamini zaidi wachezaji chipukizi katika kikosi chake hicho. Kiungo huyo aliendelea kusema kuwa amekuwa akiifuatilia Arsenal karibu michezo yote wanayocheza mwishoni mwa wiki hivyo anaamini msimu wanaweza kufukuzia taji la Ligi Kuu nchini Uingereza pamoja na kupoteza baadhi ya nyota wake. Fabregas pia alizungumzia suala la kupewa muda mchache wa kucheza toka Barcelona ilipochukuliwa na Tito Vilanova msimu huu lakini nyota huyo mwenye umri wa miaka 25 amesisitiza kuwa anaelewa kuwa yuko katika mapambano ya kupigania namba ya kudumu katika kikosi cha kwanza. Kiungo huyo amesema kuwa wakati anakuja Barcelona alijua anakuja kugombani nafasi dhidi ya wachezaji bora duniani lakini anapendelea changamoto kubwa kama hizo kwani angekuwa hahitaji angebakia Arsenal ambapo alikuwa nahodha na akichezaji karibu kila mchezo.