Baadhi ya abiria walionusurika wakiwa katika eneo la tukio kabla ya kupata msaada
WANAKWAYA
12 raia wa Kenya wamekufa papo hapo jana baada ya magari waliyokuwa
wakisafiria kupata ajali katika Kijiji cha Makole jirani na Mto Wami na
kuhusisha magari manne.
Katika
tukio la ajali, wanakwaya hao 12 walikufa na wengine 25 walijeruhiwa
vibaya baada ya magari manne yakiwemo mawili ya abiria yaliyowabeba
wanakwaya hao kupinduka na lingine kugongwa na lori ambalo nalo
liligonga lori lingine baada ya kusababisha ajali hiyo.
Aidha
habari kutoka nchini Kenya zinapasha kuwa Rais wa Kenya, Mwai Kibaki
ametuma ndege ya kuwabeba majeruhi wa ajali hiyo na kuwakimbiza Kenya
kwa matibabu zaidi.
Akizungumzia
chanzo cha ajali, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Pwani, Ernest Mangu
alisema ajali hiyo ilitokea saa 11 alfajiri jana ambapo lori la mizigo
lililokuwa likitokea Tanga kuelekea Dar es Salaam liligonga basi dogo
la abiria lililowabeba wanakwaya hao waliokuwa wakitokea Nairobi kwenda
Dar es Salaam kwa shughuli za kidini.
Kamanda
Mangu alisema lori hilo lililigonga basi hilo dogo baada ya basi hilo
kusimama ili kutoa msaada kwa wanakwaya waliokuwa kwenye basi lingine
lililokuwa mbele ambalo liliacha njia na kupinduka upande wa kulia wa
barabara hiyo kwa chanzo ambacho bado kujulikana.
“Basi
hilo lilisimama na abiria waliteremka ili kutoa msaada kwa wenzao ambao
basi lao lilikuwa limepinduka upande wa kulia wa barabara ukitokea
Tanga. Wakati wakiendelea kufanya uokozi ghafla likaja lori lililokuwa
linatoka Tanga kwenda Dar es Salaam likaligonga basi lile dogo
lililokuwa limesimama.
“Wakati
dereva wa lori anajaribu kulimiliki lori hilo ili litulie barabarani,
ghafla alijikuta kigongana uso kwa uso na lori lingine ambalo lilikuwa
likitokea Dar es Salaam kuelekea Arusha.
Tukio
hilo limesababisha wanakwaya 11 ambao ni raia wa Kenya kufa papo hapo
na wengine 25, kujeruhiwa vibaya,” alisema Kamanda Mangu.
Kamanda
huyo alisema kutokana na ajali hiyo, magari yaliyokuwa yakisafiri kati
ya Dar es alam na mikoa ya Kaskazini zikiwemo pia nchi jirani za Kenya
na Uganda yalishindwa kupita katika neo hilo kutokana na malori hayo
kufunga njia na hadi jana mchana jitihada za kuyaondoa malori hayo
zilikuwa zinafanywa.
“Tunaendelea
kutafuta ufumbuzi ili kuyaondoa malori hayo na magari yaweze kupita,
tuna hakika wa kukamilisha kazi hiyo mchana huu,” alisema Kamanda Mangu.
Kuhusu
marehemu waliokufa katika ajali hiyo, Kamanda Mangu alisema walipelekwa
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili huku majeruhi wakikimbizwa katika
Hospitali ya Tumbi, Kibaha na wengine Hospitali ya Taifa ya Muhimbili
kwa matibabu zaidi.
Taarifa
tulizopata baadaye zilisema kwamba majeruhi waliofikishwa Kibaha nao
walipelekwa Muhimbili baada ya kufanyiwa huduma za kwanza. Alisema
dereva wa lori aliyeligonga basi hilo dogo la abiria anashikiliwa na
polisi kwa mahojiano zaidi.
Wakati
huo huo, habari kutoka Kenya, zilizopatikana jana zilisema Rais wa
Kenya, Mwai Kibaki ameagiza ndege za nchi hiyo kuja Tanzania kuwabeba
majeruhi na kuwakimbiza katika hopitali za Kenya kwa matibabu zaidi.
Hata hivyo habari hizo hazikueleza ni lini ndege hizo zitawasili nchini ili kuwachukua majeruhi hao.