Sitta: Elimu Na Afya Bure Inawezekana

WAZIRI wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta amesema Serikali kutoa huduma ya Elimu na Afya bure inawezekana ikiwa tu mianya ya rushwa na ufisadi itadhibitiwa ipasavyo na wananchi wataweza kunufaika na rasilimali zilizopo nchini.
Sitta alisema ni lazima turudi kwenye misingi ya uadilifu, kujali wanyonge, kukataa rushwa na kukataa ufisadi wa aina yoyote ndipo tutaweza kukusanya na kuinua uchumi wa kutosha na kulipana mishahara mizuri, kumlipa pensheni mzee na kutoa huduma hizo bure.

Aliyasema hayo alipokaribishwa katika mkutano wa akinamama wajane kutoka wilayani Karagwe na Kyelwa mkoani Kagera na kuwashirikisha wazee wa Wilaya hizo uliofanyika katika ukumbi uliopo katika ofisi za CCM wilayani Karagwe.

Sitta alisema itakuwa ndoto za kupata huduma hizo bure kama nchi haitafanikiwa kuziba mianya yote ya rushwa na wananchi wataendelea kupiga kelele wakitaka kupatiwa huduma hizo bila ya mafanikio.

“Ningependa kuwaambia wananchi, najua karibu wote tunataka utoaji wa huduma ya afya, elimu ya kuanzi msingi mpaka elimu ya juu kuwa bure, ndugu zangu katika hali ambayo hata huduma ya afya ya kawaida haipatikani ni mtihani mkubwa kwa kutoa elimu ya bure,” alisema.

Aliongeza, “Hatuwezi kuwa na nchi ina kila kitu, tunayo makaa ya mawe, maziwa, mito, bahari, madini, gesi, mbuga za wanyama, Mlima Kilimanjaro na tuna hekta za kilimo zaidi ya milioni 88, tunataka Watanzania muamke na muache kushabikia rushwa ndogo ndogo tuingie katika utamaduni unaotuwezesha kujenga heshima ya nchi yetu kwa kujali uongozi ulionyooka na wenye uhadilifu.”

Sitta alisema wananchi wasiwe na ndoto ya maisha bora kwa kila mtanzania ikiwa rushwa na ufisadi utaendelea kutawala na kufumbiwa macho.

"Ndugu zangu hatuwezi kupata maisha bora kama kiwango cha rushwa, ufisadi na dhuluma kikiwa hivi hivi tunavyokiona hivi sasa, kwa sababu Serikali ilileta utoaji pembejeo kwa kutumia vocha sasa tutaendelea vipi kama vocha zenyewe zinachakachuliwa?" alihoji.

“Iwapo tutadhibiti mianya ya ufisadi na rushwa, nchi yetu itainuka na kuweza kuwasaidia wazee wetu, wajane, watoto yatima kwa kuwapatia huduma nyingi nzuri, ilimpadi tu ufisadi unatakiwa kupigwa vita kuanzia chini huku,” alisema Sitta.

Sitta pia aliwaomba wajane hao na wazee kupita kila mahali na kuwashaui wananchi wao wakiwemo na wana CCM kuwa makini wa watu wanaojitokeza kuwania nafasi mbalimbali za kisiasa na kiserikali wasije wakafanya makosa kuwaweka watu wenye nia mbaya na nchi hii kwa kujali matumbo yao na familia zao.

“Sasa hivi hata kule bungeni mnaona baadhi ya mawaziri, anatokea mtu amekuwa waziri ndani ya miaka 2 au chini ya hapo unasikia kanunua nyumba Mikocheni ya mabilioni, haiwezekani na wala haingii akilini hakuwa waziri wa wananchi huyu ameingia kuchuma tu,” alisema.

Waziri Sitta amemaliza juzi ziara ya kiserikali ya siku tano mkoani humo alipokuwa akiangalia miradi mbalimbali inayohusiana na muingiliano wa uchumi na kijamii kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). 
Gazeti Mwananchi jumapili