Taarifa Kwa Umma- Jeshi La Polisi Lakanusha Watoto Kuhudhuria Shule Wakiwa Gerezani Kwimba


JESHI LA MAGEREZA LAKANUSHA HABARI YA WATOTO KUHUDHURIA SHULE WAKIWA GEREZANI KWIMBA.
Na: Veronica Kazimoto – MAELEZO

Dar es Salaam

4/09/2012.

Jeshi la Magereza nchini limekanusha habari kuwa kuna watoto katika Gereza la Wilaya ya Kwimba wanaoenda shule na kurudi gerezani kuungana na familia yao.

Taarifa iliyotolewa na Kaimu Kamishna Jenerali wa jeshi la Magereza nchini Fideli Mboya, kufuatia habari iliyotolewa na Gazeti moja la kila siku hapa nchini, kuwa kuna watoto Gereza la Kwimba ambao wanahudhuria masomo huku wao na wazazi wao wakiwa gerezani.

“Yote yaliyoelezwa kwenye habari hiyo yana ukweli isipokuwa suala la watoto kuhudhuria masomo wakati wakiwa gerezani,ukweli ni kwamba hakuna watoto wanaotoka gerezani hapo kwenda shule na kurudi gerezani”, imeeleza taarifa hiyo.

Taarifa hiyo ya jeshi la Magereza nchini imeeleza kuwa, kuna familia ya watu watano baba, mama na watoto watatu wenye umri wa miaka 20, 19 na 1 ambao wote ni washtakiwa wa kesi ya mauaji isipokuwa huyo wa umri wa mwaka mmoja.

Katika taarifa yake kaimu Kamishna Mboya ameeleza kuwawatuhumiwa wote wapo gerezani wakisubiri upepelezi wa kesi yao ya mauaji inayowakabili ukamilike na hakuna kati yao anayetoka nje ya gereza na kurudi kama mtu huru.

Jeshi la Magereza nchini limelazimika kutoa ufafanuzi wa taarifa hii kufutia mbunge wa viti maalum mkoa wa Mwanza Leticia Nyerere kufanya ziara katika gereza la wilaya ya Kwimba na taarifa za ziara hiyo kuchapishwa katika gazeti moja la kila siku hapa nchini.