Cheka Na Chimwemwe Kukutana Tena Addis Ababa

                                    
                TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Nchini (TPBC) tayari imemtafutia bondia Francis Cheka mpambano wa marudiano kati yake na bondia Chiotra Chimwemwe wa Malawi katika jiji la Addis Ababa, Ehtiopia.

Mpambano huo utafayika January 26, siku ya ufunguzi wa mkutano wa wakuu wa nchi za Africa (AU Summit) katika jiji hilo la Wafalme la Abesinia!

Cheka na Chimwemwe watakutana jijini Arusha Desemba 26 (Boxing Day) katika mpambano wa kutafuta nani mbabe wa uzito wa Super Middle katika bara la Afrika, Mashariki ya Kati na Ghuba ya Uajemi (IBF AMEPG). Katika mpambano huo mafahali hawa wawili wataumana kiume kwa raundi 12 za dakika tatu kila mmoja!

Mpambano wa Cheka na Chimwemwe jijini Arusha umeandaliwa na kampuni ya Screen Hills (T) Investment ya jijini Dar-Es-Salaam inayomilikiwa na promota maarufu aliyewahi kuwa bingwa wa taifa katika ngumi za ridhaa na kulipwa Andrew George aka Chagga Boy!

Umaarufu wa wawili hawa umewafanya mapromota wanaoandaa tamasha la kuchangisha pesa kwa ajili ya kulisha watu wenye njaa katika bara la Africa kuwaingiza Cheka 26(15)-6(3)-1 na Chiotra 26(15)-4(2)-1 katika mpambano hwa marudiano utakaofanyika jijini Addis Ababa, Ethiopia tarehe 26 Januaru 2012!

Katika tamasha hilo, pambano kuu litakuwa kati ya bondia Oliver McCall 56(37)-12(1)-0 kutoka Marekani ambaye aliwahi kuwa bingwa wa uzito wa juu duniani akipambana na bondia Sammy Retta - 18(17)-3(2)-0 kutoka Ethiopia kugombea ubingwa wa IBF Africa, Mashariki ya Kati na Ghuba ya Uajemi (IBF AMEPG) katika uzito wa juu (Heavy weight)

Mapambano mengine yatawakutanisha mabondia Daniel Wanyonyi 14(12)-5(2)-2 wa Kenya atakayechuana na bondia Issac Hlatswayo 30(10)-5(3)-1 kutoka Afrika ya Kusini katika kugombea ubingwa wa IBF Afrika, Mashariki ya Kati na Ghuba ya Uajemi (IBF AMEPG) katika uzito wa Welterweight
Naye Manzur Ali 7(4)-8(3)-0 bingwa wa uzito wa juu kutoka nchi ya Misri atachuana vikali na bondia Harry Simon 27(20)-0-0 kutoka Namibia ubingwa wa IBF Afrika, Mashariki ya Kati na Ghuba ya Uajemi (IBF AMEPG) katika uzito wa Light heavyweight.

Mpambano huu umeidhinishwa na Shirikisho la Ngumi la Kimataifa (IBF) na Cheka kupewa kibali na Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Nchini (TPBC).

Imetolewa na:
Onesmo A,M, Ngowi
Rais, TPBC
Rais, IBF /Africa