Uzinduzi Wa Mashujaa Show
BENDI
ya Wenge BCBG usiku wa kuamkia janao ilikonga nyoyo za mashabiki wa
muziki wa dansi waliofika kwenye viwanja vya Leaders Club kushuhudia
uzinduzi wa albam ya pili ya Bendi ya Mashujaa ya Risasi Kidole, huku
matatizo ya kiufundi yakisababisha bendi ya Mashujaa kushindwa kuzindua
albamu hiyo.
Pamoja na kuchelewa kuanza kwa shoo hiyo, kutokana na matatizo ya
kukatika kwa umeme kila muda, JB Mpiana alianza kuwatanguliza wanamuziki
wake wakiongozwa na mmoja wa waanzilishi wa bendi hiyo, Shai Ngenge, na
kupiga sebene kabambe kabla ya kufuatiwa na wimbo wa zamani wa Kinie
Bouger, ambao enzi zake alishirikiana na akina, Ngiana Makanda, miaka
ya katikati ya 1990.
Wimbo huo uliweza kuondoa kero kwa mashabiki hao na kuwasahaulisha yale
yaliyokuwa yakiwatokea wanamuziki wa Mashujaa, ambao kila walipokuwa
wakipanda jukwaani na wanapofika kuanza sebene umeme unakatika, jambo
lililowafanya kupanda jukwaani mara nne, lakini wakishindwa kumaliza
wibo mmoja tu wa Risasi Kidole.
JB Mpiana alionekana kuwa ni mkombozi kwa mashabiki wachache waliokuwa
wamebaki huku wakipiga moyo konde kuwa hawataondoka viwanjani hapo bila
ya kumuona JB, katika uzinduzi huo kutokana na burudani safi.
Kitu ambacho kiliwashangaza mashabiki wengi ni kutokatika kwa mara kwa
mara kwa umeme kama ilivyotokea kwa bendi ya Mashujaa ilipokuwa
jukwaani. Mpiana aliweza kufanya kweli katika shoo hiyo kwani umeme
haukukatika mpaka aliposhuka jukwaani majira ya saa 10 alfajiri.
Katika shoo hiyo, Mpiana aliweza kupiga nyimbo mbali mbali za zamani
ikiwa pamoja na Barakuda, Djodjo Ngonda, Walay Danico, Dizo Dizo na zile
mpya katika mtindo wa non-stop.
Mashujaa ndio walikuwa wa kwanza kupanda jukwaani na mara walipoanza
kucheza shoo ya ufunguzi ambao imewajumuisha wanenguaji wa kike na wa
kiume na waimbaji, umeme ulikatika na kazi ya kuanza kurejesha ikaanza
na kuchukua muda wa dakika zisizopungua 30.
Tatizo hilo liliendelea mara kwa mara huku bendi hiyo ilishindwa
kumaliza tatizo hilo na jitihada za kutatua hazikutoa jibu la mara moja,
huku Mmoja wa viongozi wa Bendi hiyo, King Dodoo, akionekana kuhaha
kila kona ya uwanja huo akiwa na Babu aliyekuwa akijitahidi kusoma dua
ili Jenereta hilo liweze kufanya kazi bila kusumbua.
Mafundi walijitahidi sana na mara baada ya mashabiki kutaka JB Mpiana
apande, mafundi walitatua tatizo hilo na kumwezesha mwanamuziki huyo
kufanya shoo bila tatizo hadi alipomaliza ratiba yake.
Katika tukio jingine lililojitokeza viwanjani hapo ni Mkurugenzi wa
bendi hiyo, Mama Sakina, aliyeanguka ghafla, ikieleza ni presha ya
ghafla kutokana na kile kilchokuwa kikiendelea mahala hapo na kukimbizwa
hospitali kwa matibabu.
Uongozi wa bendi ya Mashujaa ulisema kuwa watafanya uzinduzi mwingine
katika tarehe ambayo itatangazwa hapo baadaye.