SHAROMILIONEA NA SABABU ZA KUTOONEKANA KATIKA MOVIE ZA KIBONGO

Mzee Majuto na Sharo Milionea.
Baada ya zaidi ya miezi mitano ya staa wa movie Sharo Milionea kutoonekana kwenye movie mpya za Comedy wala kuonekana kwenye vituko show, maswali ya fans yamezidi kuwa mengi.


Yako maswali mengi, lakini moja ambalo limejirudia kwa watu wengi ni kutaka kufahamu kama kweli Sharo Milionea amejiondoa kwenye kampuni ya Al Riyami aliyoingia nayo mkataba kwa ajili ya kurekodi movie zake.

Jibu alilolitoa Sharo ni kwamba kwa sasa amejiweka pembeni kwanza kutokana na sababu za kimaslahi ila hajaondoka wala kugombana na boss wake, analilia maslahi yake ndio maana haonekani kwenye movie sasa hivi.

Amesema “Bado naendelea kumsikiliza boss kwa sababu bado hatujafikia muafaka wowote japo ni zaidi ya miezi sita toka ameniambia tutaongea kesho, sasa hivi nimekua mtu mkubwa na majukumu yameongezeka sasa inabidi na kipato kiongezeke kwa sababu tunafanya kazi kubwa ndio maana nilikaa na boss wangu kumwomba aniongezee kipato, hapo sasa ndio pakawa pana utata, mimi mpaka leo watu wanajua nina gari, wengine wananiomba msaada wakijua nitawasaidia kwa sababu nina pesa kumbe sio”

Sharo amesema sasa hivi anahitaji kulipwa milioni tatu kwa movie moja na sio tena pesa ndogo ambayo wanalipwa wakati movie huwa zinaingiza mpaka milioni 50 lakini wako watu mpaka leo hii wanalipwa laki mbili, mbili na nusu na kupata umaarufu kunuka ambao hausaidii- ameongea Sharo Milionea.

Sharo Milionea amethibitisha kujipanga zaidi kimuziki na ndio maana leo ameachia Audio ya single yake mpya aliyofanya na Dully Sykes inaitwa Chuki ni bure, single ambayo video yake imeshaanza kuonekana kwenye Tv tayari.