Neville Meena, Dodoma
NAIBU Spika wa Bunge, Job Ndugai amemwadhibu Mbunge wa Kigamboni (CCM),
Dk Faustine Ndungulile kutohudhuria vikao vitatu mfululizo baada ya
kushindwa kuthibitisha tuhuma kwamba madiwani wa Halmashauri ya
Manispaa Temeke walihongwa ili kuukubali Mradi wa Mji Mpya wa
Kigamboni.Ndugai alitumia kifungu cha 73 (3) ambacho kinampa mamlaka ya
kumwadhibu mbunge aliyeshindwa kuthibitisha tuhuma alizozitoa, huku
pia akiwa amekaidi kufuta kauli yake kuhusiana na tuhuma hizo.
“Kwa kutumia kifungu namba 73 cha Kanuni za Bunge, hutahudhuria vikao
vya Bunge mara tatu mfululizo, askari mtoeni nje,” aliagiza Ndugai.
Awali, Dk Ndungulile alishtakiwa na madiwani wanne wa Kigamboni kwamba
aliwatuhumu kupewa rushwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, ili waunge mkono mradi wa kuendeleza
mji huo mpya wa Kigamboni.
|