MWANAFUNZI AOZA AKIFANYIWA MAOMBI KANISANI


Sifa Brown.

MWANAFUNZI wa kujitegemea wa kidato cha pili (Qualifying Test) katika Kituo cha Calvary kilichopo katika mji mdogo wa Mbalizi, Mbeya Vijijini, Sifa Brown (19) (pichani), amenusurika kufa baada ya majeraha aliyoyapata kwa kuungua na maji ya moto kuanza kuoza kutokana na kutopelekwa hospitalini, badala yake wazazi wakawa wanamfanyia maombi kanisani.

Kwa mujibu wa watu wa karibu wa familia hiyo, baada ya kuungua vibaya sehemu za mikono, kiwiliwili na mgongoni, Sifa aliyekuwa anaishi na baba yake mkubwa, Ambokile Abraham, alifichwa ndani ambapo mlezi wake huyo akishirikiana na waumini wa Kanisa la Uamsho wa Roho lililopo eneo la Simike jijini hapa, walikuwa wakimfanyia maombi.
Licha ya kufanyiwa maombi, Sifa hakupata nafuu yoyote ambapo inaelezwa kuwa majeraha yake yalianza kuoza huku mlezi wake akishikilia msimamo kuwa hakuna haja ya kwenda hospitali kutokana na imani ya dini yao.
Baada ya wasamaria wema kugundua kilichokuwa kinaendelea, walitoa taarifa kwa vyombo vya dola ambapo polisi walivamia nyumbani kwao, wakamkamata mlezi wake na kumpeleka Sifa hadi katika Hospitali ya Ifisi, Mbeya, Juni 11, mwaka huu ambapo binti huyo alianza kupatiwa matibabu.
Uwazi lilimfuata Sifa hospitalini ambapo Msemaji wa Hospitali ya Ifisi, Goodluck Lession, alikiri kumpokea mgonjwa huyo akiwa ameanza kuoza kwenye majeraha yake na kusema kuwa wanajitahidi kwa kadiri ya uwezo wao kunusuru maisha yake ingawa alicheleweshwa sana kufikishwa hospitalini hapo.
Naye Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanawake wa Jeshi la Polisi mkoani Mbeya, Mary Gumbo, aliwataka wananchi kufichua vitendo viovu vinavyofanywa na baadhi ya watu kwa watoto wanaowalea na kuongeza kuwa wanamshikilia Ambokile na mkewe kwa kitendo hicho cha ukatili na ukiukwaji wa haki za binadamu.
Uchunguzi uliofanywa na UWAZI umebaini kuwa mwanzilishi wa kanisa hilo alikwa ni Mchungaji Nise Mwasomola ambaye alifariki Februari 12 mwaka 2010 na kanisa hilo sasa linaongoza na kamati, ambapo Ambokile ni mmoja wa wanakamati.
Binti huyo alifikishwa hospitalini Ifisi Juni 11 mwaka huu na hali yake kwa sasa anaendelea vema baada ya kuanza kupatiwa matibabu.
Kwa upande wake msemaji wa Hospitali ya Ifisi, Goodluck Lession,alisema: “Tunafanya kila jitihada ili binti huyu apone ingawa alicheleweshwa sana kufikishwa hapa.”
Mwenyekiti wa mtandao wa wanawake wa jeshi la polisi mkoani Mbeya Mary Gumbo, aliyemuona binti huyo amewataka wananchi kufichua vitendo viovu vinavyofanywa na baadhi ya wanawake kwa watoto wanaowalea.
Jeshi la polisi linamshikilia Ambokile Abraham na mkewe kwa kitendo hicho cha ukatili na ukiukaji wa haki za binadamu kwa kisingizio cha imani ya kidini.

Chanzo global publisher