Shangwe Na Majonzi Kwenye Mapokezi Ya Dr Ulimboka Alipowasili Nyumbani

 
Na, Waandishi wa Globalpublishers
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini Tanzania, Dkt. Ulimboka Stephen, amerejea salama nchini leo mchana na kutoa shukrani za dhati kwa Watanzania kwa dua na michango yao kuinusuru afya yake na kuahidi kuendeleza mapambano dhidi ya huduma bora za afya na maslahi kwa Madaktari.

Dkt. Ulimboka, aliwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Kambarage Nyerere, saa 8:00 mchana na ndege ya Shirika la SA Airways, akitokea nchini Afrika Kusini, alipokwenda kwa matibabu.

Madaktari wenzake, ndugu, jamaa, marafiki, Wanaharakati na wananchi wengine, walimlaki kwa shangwe, hoihoi, nderemo huku wakiwa na mabango yenye ujumbe ambao GlobalPublishers.info imenukuu kuwa ulisomeka:

“DR. Ulimboka karibu nyumbani.”
“DR. Ulimboka, damu yako iliyomwagika inaamsha ari ya wananchi kudai haki ya afya.”
“DR. Ulimboka wewe ni mpigania haki ya afya bora kwa wananchi wote. Mungu na Watanzania wote tuko nawe.”

Kwa upande mwingine, Dkt. Ulimboka baada ya kukuta umati mkubwa uwanjani, alishindwa kujizuia, hivyo akatoa machozi kisha akasema: “Nawashukuru sana Watanzania kwa kuwa pamoja na mimi kwa maombi, sasa nimerejea nikiwa na afya njema, mapambano yanaendelea,” na kuongeza: “Watu wacheze na watu lakini wasicheze na Mungu, hasa Mungu wangu mimi.”