Sakata La Wamachinga Na Viwanja Arusha


Picha Na Woinde Shizza,Arusha  Wafanyabiashara ndogo ndogo maarufu kama wamachinga jijini Arusha leo wamezua tafrani kubwa baada ya kuvamia  eneo la kiwanja cha Ermoil lililopo mkabala na soko la Kilombero na  kuanza kugawana maeneo ya kufanyia biashara kwa kujipimia.Katika vurugu hizo mfuasi  mmoja wa  chama cha Wananchi CUF, Athuman Abrahaman, alishambuliwa kwa mawe na kisha kujeruhiwa eneo la usoni na watu wanaodhaniwa kuwa ni wafuasi wa Chadema huku gari la matangazo la Cuf  nalo likijikuta likipopolewa kwa mawe  na spika zake kuharibika vibaya.

Askari wa jiji la Arusha walionekana majira ya saa 3;30 asubuhi akipita na gari lao katika maeneo mbalimbali ya jiji hapa huku wakiwatangazia wamachinga wote kuondoka katika maeneo ambayo hayajatengwa kufanyia biashara zao.

Askari hao walikuwa wakiwatangazia wamachinga hao kuondoka katika maeneo ambayo hayajatengwa kufanyia biashara huku wakitamka ya kwamba endapo wakikahidi watachukua bidhaa zao kwa nguvu na kuwachukulia hatua za kisheria.

Baadaye  askari hao walianza kutekeleza majukumu yao ya
kusomba bidhaa hizo na kisha kuzipakia ndani ya gari lao wakivipeleka katika ofisi za manispaa ya Arusha. Hatua hiyo iliwapelekea wamachinga hao kujikusanya kwa pamoja na kisha kuvamia ghafla eneo la wazi wa Ermoil kwa kuvunja uzio wa mabati uliokuwepo na kisha kuanza kujigawiana  maeneo kwa kuyapima kwa kamba.

Wamachinga hao zaidi ya 200 walivamia huku wengine wakitumia nafasi hiyo kupora mali mbalimbali zilizopo
ndani ya eneo hilo kama mabati,nondo na saruji zilizokuwa ni mali za mtu anayedaiwa kumiliki eneo hilo.

Katika heka heka za kugawana viwanja ndani ya eneo hilo wamchinga hao walikata miti iliyokuwemo ndani na kisha kuanza kuichoma kwa moto hali ambayo ilisababisha wingu zito la moshi kutanda hewani.

Wakati  tafrani hiyo ikiendelea polisi waliokuwa wamesheheni kwenye magari yao walikuwa wakipita mara kwa mara kuzunguka eneo hilo lakini hawakuonekana wakifanya udhibiti wowote zaidi ya kuwaangalia wamachinga hao.

Mkuu wa wilaya ya Arusha,John Mongella alilaani tukio hilo na kusema kwamba wamachinga hao wamevamia eneo
hilo kimakosa kwa kuwa si la kwao huku akikitupia lawama chama kimoja cha siasa hapa nchini kwamba kimehusika katika kuhamasisha vurugu hizo.

Alisema kwamba kwa sasa watakutana kujadili tukio hilo kwa undani kwa kuwa wana ugeni mkubwa lakini alisema kwamba kitendo cha wafuasi wa Chadema kupiga mawe gari la Cuf na mfuasi wake si cha kiungwana.

Kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya manispaa ya jiji la Arusha,Omary Mkombole alisema kwamba kitendo cha wamachinga hao kuvamia eneo hilo ni kuvunja sheria na wataondolewa hapo hivi karibuni.

Mkombole,mbali na kulaani tukiohilo alisema kwamba uongozi wa jiji umepanga maeneo mbalimbali ya kufanyia biashara na eneo hilo ni mali ya mtu binafsi ambapo alikuwa ameanza jitihada za kuliendeleza