SHEIKH PONDA AONDOLEWA HOSPITALI NA KUPELEKWA GEREZA LA SEGEREA.....WAKILI WAKE ALAANI TUKIO HILO


Wakili Nassor Jumaa anayesimamia Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislam nchini, Sheikh Ponda Issa Ponda (54) ambaye kwa sasa anakabiliwa na kesi mpya ya kufanya uchochezi katika maeneo mbalimbali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amezungumzia kitendo cha kumhamisha mteja wake kutoka hositalini hadi Segerea.

Leo hii majira ya saa 7 mchana nje ya viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar  es Salaam amesema kuwa amesikitishwa na hatua  ya vyombo vya dola kumuondoa Sheikh Ponda aliyekuwa amelazwa katika wodi ya Kitengo  cha Taasisi ya Tiba  ya Mifupa  na Upasuaji wa Mishipa ya Fahamu (MOI) alikokuwa akipatiwa matibabu na kisha kumhamishia katika gereza la Segerea.


Wakili Jumaa amesema amesikitisha na kitendo hicho kwani muda mfupi baada ya wakili mwandamizi wa serikali Tumaini Kweka kumaliza kumsomea Sheikh Ponda shitaka linalomkabili, Hakimu Hellen Riwa alitoa amri ya kukaa chini ya ulinzi Sheikh Ponda aendelee na matibabu.

Jumaa akaongeza  kuwa   ameshangazwa kuona leo, wanausalama wamemtoa Sheikh Ponda wodini na kumpeleka katika gereza la Segerea na kwamba atalazimika kurudishwa tena mahakamani siku kesi yake itakapojatwa Agosti 28 mwaka huu, ambapo upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.

“Kwa kweli kitendo hicho kime nisikitisha na kunishitua sana… ila tunatafakari ni hatua gani za kisheria tutazichukua huko siku za usoni,”alisema Jumaa.

 Kwa upande wao familia ya Sheikh Ponda wamesema wanalaani kitendo kilichofanywa na serikali cha kumuondoa ndugu yao hospitalini huku akiwa anaendelea kupata matibabu.

Msemaji wa familia hiyo Is-haq Rashid, alisema kutokana na hali hiyo kama familia wanalirudisha suala la Sheikh Ponda kwa uongozi wa jumuiya na Taasisi za kiislamu kwa ajili ya hatua zaidi ya kuhakikisha kiongozi mwenzao anakuwa salama.

“Uporaji huu wa mgonjwa unazidi kutupa mashaka juu ya dhamira ya serikali hasa ikiwa tunalituhumu jeshi la polisi katika kumdhuru Sheikh,hatujui kwanini kila wakati wanafanya mambo yao kwa kuvizia kama mwanzoni tuliwaomba viongozi wenzie wawe na subira juu ya yaliyotokea sasa tunaachia hili walizungumzie wao.”alisema Is-haq.


Wakati huo huo taarifa zilizopatikana zinaeleza kuwa viongozi wa Jumuiya na Taasisi zaKiislamu  walikuwa katika kikao kizito cha kujadili hatua hiyo ya kuporwa kwa Sheikh Ponda akiwa katika matibabu 


-Via  wavuti