UHABA WA MADARASA KERO KWA WANAFUNZI NA WALIMU WILAYANI NAMTUMBO

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi KIDUGALO,Wilayani Namtumbo,Mwl. Owini Mpangala akiwa ofisini kwake.
mojawapo ya darasa shule ya msingi selous (Darasa la sita)-Namtumbo.

Na Vicent Mnyanyika,Namtumbo

UHABA wa vyumba vya madarasa ni moja ya changamoto kubwa inayoikabili sekta ya elimu Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma hali inayosababisha kushuka kwa kiwango cha elimu wilayani humo.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi hivi karibuni wilayani hapa baadhi ya walimu wanaofundisha katika shule za msingi wilayani Namtumbo wamesema wanatamani kuacha kazi au kuhama kutoka na changamoto nyingi zinazowakabili kwa muda bila ya kupatiwa ufumbuzi. Wanasema kuwepo kwa changamoto hizo za muda mrefu kuchangia kushusha kiwango cha elimu katika shule nyingi za mjini.

Uchunguzi uliofanywa katika shule za msingi Rwinga, Selou, Mkapa na Kidugalo zote kutoka Kata ya Rwinga umebaini shule hizo kukabiliwa na uhaba mkubwa wa vyumba vya madarasa hali inayowalazimu walimu kujenga vibanda vya nyasi ili kuwaepusha wanafunzi kukosa masomo kwa sababu ya uhaba huo wa madarasa.

Hali hiyo pia imewalazimu walimu kutumia kutumia vyumba vichache vilivyopo kwa kuwachanganya wanafunzi wa madarasa mawili katika chumba kimoja hali inayotia shaka mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi.

Mwandishi ametembelea Shule ya Msingi Kidugalo na kushuhudia zaidi ya wanafunzi 200, wa kuanzia darasa la tatu mpaka la sita wanasoma katika vyumba viwili vya madarasa huku wakiwa wamegeuziana migongo hali ambayo inachangia kushusha taaluma katika shule hiyo.

Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo ina shule za msingi 107 kati ya hizo shule 105 zinamilikiwa na Serikali na shule mbili ni za watu binafsi na mashirika ya dini.